Katika jitihada za kuhakikisha wadaiwa wote wa mikopo ya elimu ya juu wanarejesha mikopo hiyo, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza mkakati mpya ya kuwasaka wadaiwa maofisini na majumbani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa Bodi imeunda kikosi kazi kitakachozunguka kuwasaka wadaiwa katika maeneo hayo na kuwachukulia hatua stahiki.

Alisema kuwa wamefikia hatua hiyo kutokana na tabia za baadhi ya waajiri kutowasilisha makato au majina ya waajiriwa wao ambao ni wadaiwa wa Bodi hiyo, kinyume cha sheria.

“Baadhi ya watu wamekuwa wakitamba kuwa mimi watanipata wapi. Lakini kupitia mitandao ya kijamii wanatupa fursa ya kuwajua. Na mtaona kikosi kazi kitakapoanza kazi, tutakapokuwa tunaweza kuwafikia hadi majumbani kwao wanapokaa,” alisema.

“Na tunaambiwa hata wakati mzuri wa kuwapata ni muda wa ‘magharibi’, saa moja jioni, siku za Jumapili… na tumekwishafuata utaratibu huo kwahiyo itatusaidia kwa dhati,” Bosi huyo wa HESLB aliongeza.

Hatua hiyo imetangazwa na Bodi hiyo ikiwa ni mwezi mmoja tangu Bunge lifanyie marekebisho sheria ya mikopo ya elimu ya juu na kuongeza kiwango cha makato hadi asilimia 15 ya mshahara kwa waajiriwa wa sekta rasmi, na shilingi laki moja kwa wadaiwa wanaofanya shughuli binafsi.

Kupitia marekebisho hayo, mwajiri atakayeshindwa kuwasilisha jina mfanyakazi wake ambaye ni mdaiwa wa Bodi hiyo atakubwa na adhabu ya faini au kifungo kisichopungua miezi 36 jela.

Kwa mujibu wa Bodi hiyo, kati ya Julai hadi Novemba mwaka huu zaidi ya shilingi bilioni 26 zilikusanywa kutoka kwa wadaiwa. Kiasi cha shilingi bilioni 483 kimetengwa kwa ajili ya kugharamia mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/17.

Wingu zito lazidi kutanda sakata la Faru john
Wadaiwa sugu elimu ya juu kusakwa nyumba nyumba