Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuwafutia mikopo walimu wanne ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo, walionaswa kwenye kipande cha video wakimshambulia mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mbeya.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bodi hiyo imeeleza kuwa kwakuwa wanafunzi hao wamefukuzwa vyuoni kwa utovu wa nidhamu, wamekosa sifa za kuendelea kupewa mikopo na wanatakiwa kuanza kurejesha mikopo hiyo mara moja.

“Kwa mujibu wa taratibu za kukopesha, wanafunzi hao watatakiwa kuanza kurejesha kiasi walichokopeshwa mara moja,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo ya HESLB.

Imewataja walimu-wanafunzi hao na vyuo walivyokuwa wakisoma kwenye mabano kuwa ni Frank Msigwa (Chuo Kikuu cha Dar es Salam), John Deo (Chuo Kikuu cha Dar es Salam), Evance Sanga (Chuo Kikuu cha Dar es Salam) na Sante Gwamaka (Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere).

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako juzi aliagiza walimu hao wafukuzwe vyuoni kwa kosa la kumshambulia kikatili mwanafunzi huyo.

Pia, Waziri wa Nchi – Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene aliagiza Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya avuliwe madaraka yake mara moja kwa kuwa alionekana kutaka kuficha kisa hicho.

Video: Chris Brown awasili Kenya, Wananchi wataka afukuzwe kama Koffi Olomide.....
Ali Kiba ajiachia na Raila Odinga Mombasa