Bodi ya Uhuru Media inayosimamia vyombo vya habari vya Chama cha Mapinduzi(CCM) vya Uhuru Publications Limited (UPL) wachapishaji wa Gazeti la Uhuru, Mzalendo na Burudani pamoja na People’s Media Communication Limited (PMCL) inayoendesha kituo cha redio Uhuru imejiuzulu kupitia barua ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Al-haj Kimbisa.

Akitoa taarifa hiyo leo Septemba 22, 2016 Msemaji wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Christopher Sendeka ameeleza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amepokea barua hiyo ya kujiuzulu kwa bodi hiyo leo ambayo nakala yake imenakiliwa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdalrahaman Kinana.

Sendeka amesema barua hiyo inaeleza kuwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Bodi hiyo wameamua kwa hiyari yao kujiuzulu nafasi zao.

Amesema Bodi ya Uhuru Media Group ndiyo iliyokuwa na majukumu ya kusimamia, kuelekeza na kuzishauri Menejimenti ya Makampuni hayo na kubuni mbinu na mikakati ya kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa vyombo vya habari vya CCM.

 

Jipya Laibuka Sakata La Dimitri Seluk Na Pep Guardiola
Vipengele vya MTV MAMA vyatajwa, wasanii wachache TZ kushiriki