Kundi la kigaidi la Boko Haram linaripotiwa kumuua Kamanda wao mmoja mwandamizi baada ya kubaini kuwa alikuwa anapanga njama za kujisalimisha.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kilichokaririwa na vyombo vya habari nchini Nigeria, kundi hilo lilibaini kuwa Kamanda Ali Garga alikuwa anapanga kutoroka pamoja na mateka kadhaa.

Garga ambaye ni wa kabila la Fulani aliyekuwa mfugaji kabla ya kujiunga na kundi hilo na kupewa mafunzo ya kijeshi ya vita ya ardhini, anadaiwa kuwa alikuwa anapingana na kitendo cha kuwateka watu na kisha kuwatumia kubadilishana fedha na watu wao wa karibu (ransom).

“Gaga hakuwa anapenda kitendo cha kuwatumia mateka kubadilishana fedha kama masharti ya kuwaachia. Ilifikia hatua ambayo ilibainika alitaka kuondoka akaendelee na maisha yake ya ufugaji na kuungana na familia yake,” chanzo hicho kinakaririwa.

“Alipoingia Boko Haram alipewa mafunzo ya kivita na baadaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kuendesha mapigano, pamoja na kuyajua mazingira kwakuwa alikuwa mfugaji kwa muda mrefu. Walimpandisha cheo hadi ngazi ya Ukamanda (Commanding Officer,” kiliongeza chanzo hicho.

Chanzo hicho kilieleza kuwa Garga alingia matatani baada ya kundi hilo kunasa mawasiliano yake na watu wa nje ambao wangemsaidia kumuokoa kabla hajauawa.

Boko Haram wameendelea kutekeleza mauaji ya watu wasio na hatia katika eneo la Nigeria kwa kisingizio cha imani ya dini inayopinga elimu ya Magharibi.

CCM yatoa karipio kwa wanaotafuta Urais Zanzibar
Video inayoonesha mateso ya jela yawaokoa