Tukio la kulipuliwa bomu kwenye nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar, Hamdan Omar Makame limepelekea jeshi la polisi kugeuka mbogo kuwasaka wahusika.

Taarifa zilizotolewa jana kwa waandishi wa habari na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam zimeeleza kuwa tayari jeshi hilo limewakamata na kuwashikilia watu 42 wakihusishwa na tukio hilo.

Kamanda Mkadam alieleza kuwa bado msako mkali unaendelea dhidi ya watu wanaoaminika kuwa walihusika kupanga na hatimaye kutekeleza tukio hilo lililoharibu nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi visiwani humo na kujeruhi watu waliokuwa wamelala ndani ya nyumba hiyo.

“Bado tunaendelea na uchunguzi wa jambo hili na tukishakamilisha tutatoa taarifa rasmi,” alisema Kamanda Mkadam.

Juzi, majira ya saa tano usiku, watu wasiojulikana walirusha kitu kinachoaminika kuwa ni bomu lililolipua nyumba ya Kamishna wa Polisi. Tukio hilo limehusishwa na mvutano wa kisiasa unaendelea visiwani humo zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio (Machi 20).

Baadhi ya wananchi wameiambia Dar24 kuwa wamekuwa katika hali ya hofu kufuatia tukio hilo huku wakitolea mfano ulinzi uliokuwepo kwenye nyumba ya mkuu huyo wa polisi wakilinganisha na nyumba zao.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limewatoa hofu wananchi wote kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu kwani usalama utaendelea kuimarishwa muda wote visiwani humo.

Audio: Sikiliza hapa wimbo mpya wa Sugu 'Freedom'
Diamond aeleza kitu kilichomvuta Kanye West kwake na Mpango kati yao