Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango, Ufutuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kulthum Mansoor amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akikabiliwa na kesi ya uhujumu ambapo anadaiwa kujipatia zaidi ya sh. bilioni 1.4 kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.
 
Mshtakiwa huyo anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka kwa wafanyakazi wenzake. Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali Wankyo Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kelvin Mhina kuwa katika tarehe tofauti za Januari 2013 na Mei 2018, mshtakiwa alighushi barua ya ofa ya tarehe 13 Agosti 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa, barua hiyo imetolewa na Halmashauri ya Wilaya Bagamoyo huku akijua kuwa si kweli.
 
Aidha, katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu imedaiwa, kati ya Januari 2012 na Mei 2017 huko Upanga Wilaya ya Ilala jijini Dar es Saalam mshtakiwa kwa kudanganya alijipatia jumla ya sh. milioni 32.2 kutoka kwa watu sita tofauti tofauti kama malipo ya viwanja tofauti vilivyoko Wilaya ya Bagamoyo katika kijiji cha Ukuni kwa kujifanya kuwa yeye ni mmliki wa viwanja hivyo huku akijua kuwa sio kweli.
 
Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka kwa Alex Mavika ( milioni Sh.5.2), Wakati Katondo, (milioni 3), Gogo James, (milioni Sh.5), Ekwabi Majungu, (Sh.milioni 7) John Amos (Sh.milioni 7) na Rose Anatory, (Sh.milioni 5), ambao wote ni wafanyakazi wa taasisi hiyo.
 
Pia, katika shtaka la mwisho imedaiwa kati ya Januari 2013 na Mei 2018 huko Upanga, mshtakiwa Kulthum alijipatia fedha Sh.1,477,243,000 wakati akijua kuwa fedha hizo ni haramu na ni zao la kosa Tangulizi la kughushi.
 
  • Video; NASSARI kulipa FIDIA Bunge baada ya kushindwa Mahakamani? | “Spika ametekeleza maagizo
  • Kigogo wa Takukuru kuburuzwa mahakamani
  • Kigogo wa Takukuru aliyetajwa na JPM alala mahabusu
 
Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina Mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo itatajwa tena Aprili 12, 2019

Siri mtoto wa Waziri Msuya kupata ubosi UN
Jengeni tabia ya kupima afya mara kwa mara- Samia Suluhu Hassan