Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imepitisha jina la Dkt. Tulia Ackson kuwa mgombea pekee wa nafasi ya uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Uamuzi huo umefanyika leo katika ukumbi wa White House jijini Dodoma, ambapo Kamati hiyo imepitia majina 70 ya wanachama wake waliokuwa wamechukua fomu ya kuwania kiti hicho, baada ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu.


Katibu Mwenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka amezungumza na waandishi wa habari punde baada ya kumalizika kwa kikao hicho, ambapo amesema Kamati Kuu imepitisha jina la Dkt. Tulia kama jina pekee la mgombea wa chama hicho.
Dkt. Tulia kwa sasa ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeshika nafasi hiyo kuanzia mwaka 2015.

Dkt. Tulia Ackson ni mwanasheria na mwanasiasa Mtanzania mwanachama wa Chama cha kisiasa cha Mapinduzi, aliteuliwa na Hayati, Rais John Magufuli kuwa mbunge kwa miaka 2015 – 2020, na mwaka 2020 aligombea katika Jimbo la Mbeya Mjini akashinda kuwa Mbunge kupitia CCM na akaendele pia kuwa naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

DJ maarufu Kenya ajiua kwa sumu
Wanawake wapigwa marufuku kukaa mbele kwenye malori