Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli ameagiza vyuo vyote nchini kufunguliwa kuanzia Juni 1, 2020.

Akizungumza baada ya kuwaapisha Mabalozi aliowateuwa katika nchi mbalimbali, Rais Magufuli amesema kuwa pamoja na kufunguliwa kwa vyuo, katika tarehe hiyohiyo wanafunzi wa kitado cha sita wanapaswa kurejea shuleni na kujiandaa na mitihani yao ya kuhitimu.

“Pia, vijana waliokuwa kitato cha sita, waliokuwa wanajiandaa kufanya mitihani warudi shuleni Juni 1, 2020. Na Wizara ya Elimu iandae utaratibu wa wanafunzi hao,” amesema Rais Magufuli.

Ameitaka Wizara ya Elimu na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kujiandaa katika kipindi cha siku tisa zilizosalia, kuhakikisha kuwa wanafunzi wa vyuo wanaopaswa kupata mikopo wanapata mikopo yao kwa muda ili waendelee na masomo yao katika siku iliyotajwa.

Aidha Rais Magufuli amesema kuwa kwa wanafunzi wa shule za msingi, wanapaswa kuendelea kusubiri.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameruhusu kuanza kwa michezo yote nchini, huku akisisitiza kuwa kushiriki michezo ni sehemu ya hatua za kupambana na virusi vya corona kwa kuimarisha kinga za mwili.

Hata hivyo, amesema kuwa ni vyema kukawa na utaratibu wa kuchukua tahadhari, hivyo alichelea kuruhusu mashabiki kushiriki katika michezo hiyo.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli alisema kuwa ameruhusu ndege za utalii zilizopanga kuingia nchini, kuingia kuanzia Mei 27, 2020. Alisema kuwa watalii watakaoingia hawatakaa kwa siku 14 karantini, bali watapimwa joto na kama wako vizuri wataendelea na shughuli za utalii.

Aliongeza kuwa ikiwezekana Wizara ya Utalii iweke mpango wa kujifukiza maarufu kama kupiga nyungu uwe sehemu ya utalii, na watalii nao wanaweza kupewa zawadi ya kujifukiza.

Rais Magufuli pia aliipongeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kazi nzuri waliyoifanya. Alisema kuwa Waziri wa Wizara hiyo, Ummy Mwalimu alifanya kazi nzuri.

Matumaini ya Corona kuisha duniani yaanza kufifia
Elias Maguri: Usiogope Kuanza Upya