Katika hali ambayo haikutegemewa, Mkutano kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un umevunjika.

Mkutano wa siku mbili kati ya viongozi hao waliokutana nchini Vietnam umelazimika kuahirishwa baada ya kutofautiana katika masuala ya msingi, hivyo hawakufikia lengo la kutia saini nyaraka zozote.

Waandishi wa habari walishangazwa na taarifa ya kuahirishwa kwa chakula cha mchana kati ya viongozi hao ambacho walitarajia kushiriki kuchukua matukio.

Kwa mujibu wa Rais Trump ambaye alizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa mkutano huo, mahitaji ya Korea Kaskazini na yale ya Marekani yameonekana kutoshabihiana.

“Ndoto yetu na ndoto yao havikushabihiana. Wao walitaka kuondolewa vikwazo katika maeneo yote, na hatukuweza,” alisema Trump.

“Hatujakata tamaa, kuna uwezekano. Anataka kuachana na silaha za nyuklia, [Kim] anataka kufanya kwenye maeneo ambayo yana umuhimu kidogo kuliko tunavyotaka. Wakati mwingine inabidi kuondoka na wakati huo ulikuwa leo,” aliongeza.

Hata hivyo, Trump amemuelezea Kim kama kiongozi mzuri na kwamba anaamini wakati mwingine watafikia muafaka. Amesema ingawa mkutano huo haukuzaa matunda yaliyotarajiwa, kuna hatua ambazo zimepigwa kulinganisha na ilivyokuwa awali.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amewaambia waandishi wa habari kuwa katika makubaliano ya awali walibaini kuwa hakukuwa na kitu ambacho kingeifaidisha ipasavyo Marekani.

Amesema timu ya nchi hizo mbili itakutana tena kuendelea kujadiliana kwa mara nyingine ili wafikie muafaka.

Video: Familia yatoa ratiba rasmi mazishi ya Ruge Mutahaba
Kim Jong Un aweka 'rekodi' akijibu maswali ya waandishi mbele ya Trump