Anthony Joshua amefanikiwa kurejesha mikanda minne tofauti ya ubingwa wa dunia uzito wa juu usiku wa kuamkia leo baada ya kumpiga Andy Ruiz, katika pambano lao la marudiano lililofanyika Saudi Arabia.

Joshua alionesha kuyafanyia kazi maelekezo ya mkufunzi wake na washauri wengine wa ndondi kwa kuhakikisha anakaa mbali na Ruiz Jr. huku akijikusanyia alama kwa ngumi za mbali.

Baada ya raundi 12, Joshua alitajwa kuwa mshindi akimuacha mbali Ruiz (118-110, 118-110, 119-109). Alama hizi zimeonesha jisi ambavyo Joshua alitawala pambano kwa kuzoa alama ingawa Ruiz alikuwa akimkimbiza wakati wote.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki mitandaoni wameonesha kutofurahishwa sana na pambano hili kutokana na mtindo mpya wa Joshua wa kupiga na kukimbia, kiasi cha kuonekana kama alikuwa ameiga mtindo wa Floyd Mayweather na Wladimir Klitschko.

“Mwanaume kama mimi huwa sitafuti sababu [nikishindwa]. Haya ni masumbwi. Nimekuwa nikiwapiga watu kwa KO, nilitakiwa kujirekebisha kutokana na pambano la kwana na kupigana mtindo wa ubora wa hali ya juu. Unapaswa kupiga ngumi na kuhakikisha haupigwi,” Joshua alisema baada ya kutangazwa kuwa mshindi.

Taarifa zilizotolewa hivi punde na Shirikisho la Masumbwi Duniani (WBO), Anthony Joshua atalazimika kutetea ubingwa wake dhidi ya Oleksandr Usyk kutoka Ukrain. Pambano kati ya wawili hao linatakiwa kufanyika ndani ya kipindi cha siku 180. Usyk anaweza kuwa mpinzani mkali kwa Joshua, kwa kuzingatia kuwa hajawahi kupoteza pambano hata moja kati ya mapambano yake 17.

Katika pambano la kwanza, Ruiz alishinda kwa KO katika raundi ya saba ya pambano, baada ya kumnyanyasa Joshua kwenye raundi ya nne.

Live: Rais Magufuli akiweka jiwe la msingi ujenzi wa Meli mpya na ukarabati wa MV - Victoria
TCRA yasisitiza simu zisizosajiliwa kuzimwa Desemba 31, Wasichana waonywa kuhonga wanaume