Kufuatia mgomo wa Madereva wa Mtandaoni Tanzania (TADO) unaoendelea kwa siku mbili sasa dhidi ya kampuni ya Uber, zaidi ya madereva 50 wamenyang’anywa magari na mmiliki wa magari hayo akidai kushindwa kuvumilia hasara kubwa anayopata.

Mkurugenzi wa kampuni ya Smart Rental Car, Fredy Emmanuel ambaye ndiye mmiliki wa magari hayo amechukua uamuzi huo kufuatia mgomo wa madereva wakidai kuendelea kukandamizwa na Uber kila iitwapo leo kwa kufanya kazi ambayo haina faida.

Emmanuel amesema kuwa haoni faida ya kuendelea kufanya kazi na Uber kwani yeye aliamua kwenda benki kukopa na kuingia makubaliano na Uber kisha akawaajiri madereva lakini kila siku zinavyozidi kwenda Uber wanabadilika hali inayowafanya madereva washindwe kutimiza mikataba yao na yeye akiambulia hasara.

Amesema tangu Septemba 1, 2018 Uber wameendelea kutoa ofa ya punguzo la bei kwa abiria wake la 40% na kutokana na hali hiyo amekuwa akiingiza hasara ya milioni 5.1 ndani ya siku tatu tu.

“Nimeamua kusimamisha kazi na kuyarudisha magari yangu 50 na kuyaweka kwenye maegesho mpaka pale suluhisho litakapopatikana.” Amesema Emmanuel.

Umoja wa Madereva wa Mtandaoni Tanzania (TADO) wameweka mgomo wao wa saa 48 wakiitaka Kampuni ya Uber kusikiliza malalamiko yao kwani wamechoka kuendelea kukandamizwa kila iitwapo leo kwa kufanya kazi ambayo haina faida.

 

Kivuko cha MV. Nyerere chazama Mwanza
Video: Major Lazer wampa shavu Babes Wodumo kwenye ‘balance pon it’

Comments

comments