Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza shule zote zilizokuwa zimefungwa kama hatua za kupambana na mlipuko wa virusi vya corona, zifunguliwe Juni 29, 2020.

Akitoa hotuba yake wakati wa kuvunja Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Magufuli amesema kuwa kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali na wananchi kwa ujumla katika kupambana na virusi hivyo, sasa hivi athari za ugonjwa huo sio kubwa.

“Kutokana na kuendelea vizuri kwa mapambano dhidi ya corona, napenda nichukue nafasi hii kutangaza kuwa kuanzia tarehe 29 Juni, 2020 shule zote zifunguliwe zilizokuwa zimebaki,” amesema Rais Magufuli.

Hata hivyo, Rais Magufuli amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya virusi vya corona.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewapongeza wabunge walioendelea na vikao vya Bunge na kwamba wachache waliokimbia wanapaswa kufahamu kuwa kukimbia tatizo sio njia sahihi.

“Bunge hili kuendelea na vikao vyake kwa kawaida kama lengo la kuwatumikia watanzania, japo nafahamu wapo wachache waliokimbia, lakini sijui kama wamesharejea, lakini niseme kukimbia haikuwa jambo sahihi kwa sababu matatizo hayakimbiwi, kukimbia changamoto ni ishara ya udhaifu,” alisema Rais Magufuli.

Lakini pia kukimbia ni ishara ya uogo, lakini pia ni ishara ya kutojiamini. Siku zote njia sahihi ya kupambana na matatizo ni kukabiliana nayo, ndio maana sisi tuliamua kukabiliana na ugonjwa wa corona huku tukiwa tunamtanguliza Mwenyezi Mungu, na hadi sasa tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa,” aliongeza.

Machi 17, 2020, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliagiza Shule zote kuanzia shule za awali na vyuo kufungwa, kama hatua za awali za kujikinga dhidi ya virusi vya corona.

Mei mwaka huu, Rais Magufuli alitangaza kufungua vyuo na kuruhusu wanafunzi wa kidato cha sita kurejea shuleni kwa ajili ya kujiandaa na mitihani ya kuhitimu.

RAIS NKURUNZIZA: Kocha aliyehukumiwa kifo akaangukia URAIS, vita na mapenzi – Makala

Aubameyang aonyesha matumaini Arsenal
Ummy akemea matumizi mabaya ya simu kwa watoto "huchochea ngono"