Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro imetoa hukumu juu ya kesi ya uchochezi iliyokuwa ikimkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi ya Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda na wenzake 49 kwa kuamuru waachiwe huru mara moja.

“Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha pasipo na shaka yoyote mashtaka dhidi ya mtuhumiwa,” alisema Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Victoria Nongwa.

Mahakama hiyo imemuachia huru Sheikh Ponda na wenzake 49 baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na kutoridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Katika kesi ya msingi upande wa mashtaka uliwasilisha mahakamani hapo mashtaka matatu yaliyowasilishwa mbele ya Hakimu Mkazi, Mary Moyo. Hata hivyo, Mheshimiwa Moyo alimfutia shtaka moja na kubaki na mashtaka mawili.

Sheikh Ponda alizuiwa kupewa dhamana baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi (wakati ule) kuwasilisha hati ya ombi la kumfungia dhamana Sheikh Ponda chini ya kifungu Namba 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Mwaka 2002.

Katika kesi ya msingi iliyowasilishwa mahakama hapo , Mwanasheria Kiongozi  wa Serikali, Bernard Kongola, alidai  kuwa Agosti 10, mwaka 2013, katika eneo la Uwanja wa Ndege, Manispaa ya Morogoro, Ponda aliwaambia Waislamu wasikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwa madai kuwa zimeundwa na BAKWATA, ambao ni vibaraka wa CCM na serikali.

Pia, Sheikh Ponda alikuwa anakabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa mali, wizi pamoja na uchozezi.

Ilielezwa kuwa  Sheikh Ponda ambaye anatetewa  na wakili wa kujitegemea Juma Nassor aliwaagiza waumini hao kuwa endapo watu hao watajitokeza kwao na kujitabulisha kwamba ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, wafunge milango na madirisha wawapige.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu alimtaka Sheikh Ponda na wenzake kutotenda kosa lolote la jinai baada ya kuachiwa huru.

“Unatakiwa kuwa mtu wa amani na mwenendo mwema katika kipindi chote hiki. Hutakiwi kufanya kosa lolote,” Hakimu alimwambia Sheikh Ponda.

Tyson Azima Ngebe Za Mpinzania Wake
Lowassa ashuhudia alipouawa Alphonce Mawazo