Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepandisha mishahara ya wafanyakazi wa Serikali kwa asilimia 23.3 (23%).

Taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imeeleza kuwa uamuzi huo wa Rais umetokana na kuridhia mapendekezo ya kiwango hicho cha nyongeza, yaliyowasilishwa kutokana na kikao cha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa na wataalam wa Serikali kilichofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.  

“Kutokana na hatua hiyo, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh. 9.7 trilioni kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara ya watumishi wote wa katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Taasisi na Wakala wa Serikali,” imeeleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Aidha, hatua hiyo pia inasababisha ongezeko la bajeti ya mishahara kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 kwa Sh. 1.59 trilioni ambayo ni sawa na ongezeko la 19.51% kwa kulinganisha na mwaka huu wa fedha.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mchakato wa nyongeza ya mishahara umezingatia Pato la Taifa (GDP), mapato ya ndani yanayotarajiwa kukusanywa katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na hali ya uchumi.

Tangazo hili la nyongeza ya mishahara linakuja ikiwa ni siku 14 tu tangu Rais Samia alipowasisitizia wafanyakazi nchini kuwa ‘jambo letu lipo’, akimaanisha kuwa ahadi ya nyongeza ya mishahara aliyoitoa mwaka jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ataitekeleza.

Mwanamke mwenye watoto wengi zaidi Afrika mashariki akijaaliwa kuzaa Pacha
Rais Samia aomboleza kifo cha Kiongozi wa UAE