Wabunge watatu wa chama tawala nchini Uingereza leo wamejiuzulu wakimtosa Waziri Mkuu, Theresa May na harakati zake kuhusu uamuzi wa nchi hiyo kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (Brexit).

Wabunge hao ambao ni Heidi Allen, Anna Soubry na Sarah Wollaston waliokuwa wa chama cha Conservative, wamejiunga na kundi huru la wabunge ambalo miongoni mwao kuna wabunge saba wa chama cha upinzani cha Labour.

Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa nchi hiyo inaendelea kuzihesabu siku kuelekea Machi 29 ambapo Uingereza inatarajia kujieungua rasmi kwenye Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu May amewasilisha hoja yake kuhusu mazungumzo mapya kati ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya, akitarajia kwenda jijini Brussels nchini Ubelgiji hivi karibuni kufanya mazungumzo mengine ya kile anachoamini kuwa ni kupunguza makali ya kiuchumi kutokana na uamuzi wa wananchi wa Uingereza kupitia sanduku la kura.

“Nimesikitishwa na hatua hiyo ya wabunge wetu watatu, lakini nitaendelea kufanya kile ambacho ni sahihi kwa nchi yetu kuhusu Brexit,” alisema May.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May akiwa Bungeni

Wananchi wa Uingereza walipiga kura Juni 2016 ambapo asilimia 51.9 waliamua kuwa nchi hiyo ijiondoe kwenye Umoja wa Ulaya mwaka huu, kinyume na yaliyokuwa matakwa ya Waziri Mkuu.

JPM afanya uteuzi wa Mkurugenzi TEWW
Tanzania yaalikwa maonyesho ya vipodozi China