Shirikisho la soka nchini Marekani limemtangaza Bruce Arena kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo, badala Jürgen Klinsmann ambaye jana alionyeshwa mlango wa kutokea.

Arena, anakabidhiwa kikosi cha Marekani huku akiwa anajivunia rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi ya soka nchini humo (MLS) mara tano akiwa na klabu za D.C. United na LA Galaxy.

Akiwa na D.C. United kocha huyo alitwaa ubingwa wa MLS mara mbili (1996, 1997) na alipokwenda LA Galaxy alifanikiwa kunyanyua taji hilo mara tatu (2011, 2012, 2014).

Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa kocha huyo kukabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Marekani, kwani aliwahi kuiongoza timu hiyo katika fainali za kombe la dunia za mwaka 2002 zilizofanyika Korea Kusini na Japan.

Arena, anatarajiwa kusaini mkataba wa kuanza kazi mwanzoni mwa mwezi ujao, na jukumu kubwa lililo mbele yake kwa sasa ni kuhakikisha anaisaidia Marekani kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 ambazo zitaunguruma nchini Urusi.

Kwa sasa timu ya Marekani inaburuza mkia baada ya kuanza vibaya michezo ya hatua ya mwisho ya kufuzu katika ukanda wa Amerika ya kati na kusini (CONCACAF) kwa kufungwa na Costa Rica na kutoa sare ya bila kugunga na Mexico.

Mchezo wa kwanza kwa Arena utachezwa Mwezi Machi mwaka 2017 ambapo timu ya taifa ya Marekani itawakabili Honduras katika muendelezo wa kusaka nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia.

Serge Aurier Apigwa Stop Kuingia London
CAF Yawapeleka Jela Waamuzi Wa Soka