AFISA Usalama wa Klabu ya Singida Big Stars juzi (Jumapili-Machi 26) alimtoa kiungo wa timu hiyo, Bruno Gomez kwa nguvu katika kundi la mashabiki kutokana na kila mmoja kutaka kupiga naye picha.

Tukio hilo lilitokea katika mchezo wa kirafiki kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini na kumalizika kwa SBS kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji.

Taarifa zimekuwa zikidai kuwa kiungo huyo yupo kwenye rada za klabu ya Young Africans na msimu ujao anaweza kutua kwenye kikosi hicho ili kuongeza nguvu kwenye michuano ya kimataifa.

Bruno Raia wa Brazil ameonyesha uwezo mkubwa wa kucheza nafasi tofauti uwanjani na kwa ufanisi wa hali ya juu ambapo hadi sasa ametumika kama namba sita, namba nane, namba 10 na pia winga huku akifanya vizuri katika ufungaji wa mabao na kupiga pasi za mwisho.

Fundi huyo wa upigaji mipira iliyokufa, hadi sasa ameifungia Singida Big Stars mabao tisa huku akipiga pasi za mwisho nne.

Achana na picha tu ndani ya uwanja kiungo huyo ambaye ametoka kwenye majeraha hivi karibuni alionesha uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu ambapo kila alipogusa mpira mashabiki walikuwa wakishangilia huku baadhi wakidai hiyo ni mali ya Yanga.

Mara baada ya filimbi ya mwisho ya Mwamuzi, Nassib Ahmed, mashabiki walishuka jukwaani na kumkimbilia mchezaji huyo na kuanza kupiga naye picha.

Ilibidi ofisa huyo aingilie kati na kumchomoa nyota huyo kwa nguvu na kumkimbiza katika basi huku mashabiki wakilalamika kitendo hicho wakidai bado walikuwa wakitaka wakipiga naye picha.

Hii imekuwa ikitokea kwa wachezaji wengi mastaa kwenye timu zao kwa mashabiki kutamani kupiga nao picha na kuzishea kwenye mitandao ya kijamii.

Chanzo Mwanaspoti

Robertinho afurahishwa na kiwango Simba SC
Makamu wa Rais wa Marekani kuipaisha Tanzania Kimataifa