Mlinda mlango kutoka nchini Italia Gianluigi Buffon, amewakata vilimi wanaozungumzia mpango wake wa kustaafu soka, kwa kigezo cha umri wa miaka 40 alionao kwa sasa.

Buffon ambaye kwa sasa ni mlinda mlango wa klabu bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, amesema hana mpango wa kutundika daluga katika miaka ya karibuni, na huenda akaendelea kukaa langoni mwa miaka mingine kumi ijayo (Muongo Mmoja).

Gwiji huyo ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Italia kilichotwaa ubingwa wa dunia mwaka 2006, amesema anaamini bado ana uwezo na nguvu za kuendelea kucheza soka, na kila siku anahisi bado yupo “FIT” tofauti na watu wanavyomfikiria.

“Katika miaka ya karibu nimejifunza mambo mengi sana katika mchezo wa soka, siamini kama nilichojifunza kitaweza kuwa sababu za kunisukuma pembeni na kutangaza kustaafu soka,”

“Ninaamini nina nafasi nyingine ya kucheza soka kwa miaka kumi ijayo, hakuna linaloshindikana katika mipango niliojiwekea, ninaendelea kuwa mwenye furaha kama ilivyo kwa wachezaji wengine ambao wana umri mdogo.” Amesema Buffon ambaye alifanikiwa kuitumikia timu ya taifa ya Italia katika michezo 176, kuanzia mwaka 1997 hadi 2018.

Buffon kwa sasa ameonyesha uwezo mkubwa na kufanikisha azma ya kuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain.

Buffon alijiunga na Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu uliopita akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC, ambapo alifanikiwa kuwatumikia katika michezo 509, kuanzia mwaka 2001 hadi 2018.

Video: Iokote ya Maua Sama yashika kasi, Vanessa aja kivingine
Masoud Djuma aikana Young Africans