Kasi ya kupambana na ujangili iliyoongezwa na Rais John Magufuli imeendelea kuzaa matunda huku Kikosi Kazi Maalum kilichoundwa kikiripotiwa kukamata bunduki 11 nyumbani kwa mbunge.

Kwa mujibu wa chanzo cha gazeti la Mwananchi, Bunduki hizo zinazosadikika kutumika katika matukio ya ujangili zilikutwa nyumbani kwa mbunge wa CCM ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kutoingilia unyeti wa oparesheni hiyo.

Taarifa hizo zimekuja ikiwa ni siku chache baada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi za Maliasili na Utalii na kukipa nguvu zaidi kikosi kazi hicho ambacho kilidaiwa kuanza kuzimwa.

Rais Magufuli alimtaja mtu mmoja kwa jina la ’Mpemba’ anayehusishwa na biashara haramu ya pembe za ndovu kwa muda mrefu na kueleza kuwa angeshangaa kama asingekamatwa. Alishuhudia meno 50 ya Tembo ambayo yalikamatwa kutokana na oparesheni hiyo, hali inayoonesha kuna tembo 25 waliuawa.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe juzi alieleza kuwa tayari wameshamtia nguvuni Mpemba na kwamba wanaendelea na msako wa wengine ambao wakikamatwa nchi itatikisika kutokana na majina yao.

”Hilo ni jina lake analolitumia katika harakati zake za biashara ya ujangili ili asitambulike. Yuko mwingine pia anajiita ’Mangi wa Kabila fulani’ lakini sio majina yao halisi,” alisema Profesa Maghembe na kuongeza kuwa hawaweki hadharani majina yao ili kutoharibu uchunguzi.

Profesa Maghembe aliwahakikishia Watanzania kuwa mtandao wote wa majangili utavurugwa na hakuna jangili atakayesalimika bila kujali jina lake.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alimteua Mkuu wa Majeshi wa zamani, Jenerali George Waitara kuwa Mwenyekiti wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), ambaye ameahidi kuwakomesha wafanyabiashara hao haramu.

Nelson Cabrera Aiponza Bolivia, Yashushwa Hadi Mkiani
Inter Milan Yatimiza Lengo, Yaagana Rasmi Na De Boer