Bunge la Uganda limepitisha sheria inayopinga hukumu ya adhabu ya kifo kwa baadhi ya uhalifu, na kufanya marekebisho katika sheria nne tofauti ikiwemo sheria ya kupambana na ugaidi.

Kama sheria hiyo itasainiwa na rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni, marekebisho hayo yatasitisha hukumu ya kifo.

Watunga sheria wa nchi hiyo wamesema kuwa hii ni hatua kubwa inayoweza kutokomeza hukumu hiyo, jambo ambalo mahakama ilishawahi kulipigia kelele.

Aidha, kumekuwa na kampeni mbalimbali za kutokomeza hukumu hiyo nchini Uganda, kufuatia hukumu ya mwaka 2009 ya mfungwa Susani Kigula ambaye alihoji juu ya hukumu ya kifo kuwa kinyume na katiba ya nchi.

Pia, mahakama ilitaka hukumu ya kifo isiwe lazima kwa kesi za mauaji, na kusisitiza kuwa mtu hapaswi kuwekwa jela kwa miaka mitatu wakati amehukumiwa kunyongwa, muda huo ukipita mfungwa huyo ni sawa na kwamba amepewa hukumu ya kifungo cha maisha.

Mara ya mwisho kwa rais Museveni kuidhinisha hukumu ya kifo itekelezwe ilikuwa mwaka 1999 ya watu 27 katika gereza la Luzira lililopo jijini Kampala.

Hata hivyo, ripoti ya katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hukumu ya kifo imewasilishwa katika tume ya haki za binadamu ya nchi hiyo ambapo imeeleza kuwa kuna mataifa 170 duniani yameachana na adhabu hiyo.

Benki ya dunia kuipa Tanzania dola bil. 1.7
China yatoa msimamo wake kuhusu ndoa za jinsia moja