Baada ya Kangi Lugola, kuwekwa chini ya ulinzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa madai ya ufisadi, sasa kuwekwa kikaangoni bungeni.

Nagenjwa Kaboyoka, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), amemtaka Lugola ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kutoa maelezo kuhusu sakata la ufisadi katika ununuzi wa sare za Jeshi la Polisi nchini.

Kaboyoka ametoa hoja hiyo wakati akizungumza bungeni jijini Dodoma, jana tarehe 29 Januari 2020, huku akimtuhumu Lugola kwamba alilipotosha bunge kuhusu ununuzi wa sare hizo.

“Kwa hiyo Kangi alilipotosha bunge kwa kuapa kwamba, atatoa nguo kama sare hazipo, inamaana hasomi hata taratibu,” amesema Kaboyoka.

Kaboyoka amesema Lugola akitoa maelezo hayo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atafuatilia sakata hilo, ili kujua kama idadi ya sare aliyoitoa, inaendana na idadi halisi iliyopo.

“Kuanzia hapo ndio CAG aweze kwenda stoo kujua kuna nini kutokana na zile ripoti, aone kwamba zile sare ziliagizwa mia na zimekuja mia, kinyume na hapo CAG hawezi kutoka akaenda kwenye stoo akaangalia kitu ambacho hana nyaraka zinazoonyesha kilichomo,” amesisitiza Kaboyoka.

“Nanyanyua mikono juu itakapofika jioni kama mimi nasema uongo kwamba hakuna sare hewa, najivua nguo, kamati ya mambo ya ulinzi na usalama na maofisa ya CAG twende stoo kuu tukaangalie makontena 15 na magodauni 5 yamesheheni sare za vitambaa. Nauweka uwaziri wangu rehani kama mimi nasema uongo,” Lugola aliapa bungeni.

Lugola pia alimtuhumu Profesa Mussa Assad, aliyekuwa CAG kwamba alisema uongo katika ripoti yake, juu ya ununuzi wa sare hizo.

“CAG amelihusisha Jeshi la Polisi na kashfa ya sare hewa, na kwamba sare hizi ni za bilioni 16.6. Kwa heshima na taadhima kwa moyo mkunjufu, kwa mikono yangu meupe nikiwa kama waziri makini, ambaye naitakia mema nchi hii, natetea rasilimali za Watanzania na tumuogope Mungu, sijawahi kuona mtu muongo kama CAG,” alisisitiza Lugola.

Hata hivyo kwa sasa Lugola anakabiliwa na kashfa ya kuingia mkataba wa kifisadi wa vifaa vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji vyenye thamani ya Euro Mil. 408.2 kutoka kampuni moja ya nje ya nchi ambapo atahojiwa na TAKUKURU.

Lugola anahojiwa na TAKUKURU baada ya Rais John Magufuli kuiagiza taasisi hiyo kuchunguza mkataba huo, kwa ajili ya kujua wahusika ili wachukuliwe hatua.

JPM ateua viongozi wengine, Dkt. Abbas awa Katibu Mkuu Wizara ya Habari
Waziri Mkuu atoa agizo kwa wazazi wenye watoto wanaosoma China