Bunge la Zimbabwe limemtumia barua ya wito aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe inayomtaka afike mbele ya kamati maalum ya Bunge kujieleza kuhusu sakata la madini ya almasi ya mabilioni ya fedha.

Barua hiyo inayomtaka Mugabe kufika mbele ya kamati hiyo kesho (Mei 23) ilitolewa Jumatatu wiki hii na kusainiwa na Katibu wa Bunge hilo.

“Hii ni kwa ajili ya kupata uthibitisho, ushahidi wa mdomo kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa zamani, R. G. Mugabe kuhusu mapato ya madini ya almasi,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Wabunge hao wamepanga kumhoji Mugabe kuhusu kauli yake ya mwaka 2016 kuwa nchi hiyo ilipoteza mapato ya $15 bilioni kwenye madini ya Almasi kutokana na rushwa pamoja na unyonyaji wa wageni katika sekta ya madini.

Hata hivyo, Mugabe hajajibu chochote kuhusu wito huo au kuonesha kama atahudhuria kikao hicho.

Mwanasiasa huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 94 hajaonekana hadharani tangu Novemba mwaka jana, ingawa Februari mwaka huu alifanya hafla ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa iliyofanyika nyumbani kwake.

Waziri ataka waislamu kuchukua likizo
Paraguay yafungua ubalozi nchini Israel

Comments

comments