Kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Media, Dk. Reginald Abraham Mengi kilichotokea usiku wa Mei 2 huko Dubai, leo Mei 3, 2019 bunge limeungana na Rais na Watanzania wote kuomboleza kifo cha jasiri huyo aliyegusa maisha ya watu wengi hapa nchini.

“Katika kuombeleza kifo na msiba huu mkubwa, sisi Bunge tunaungana na mheshimiwa Rais John Magufuli, familia ya marehemu na Watanzania wote kuomboleza na tukimshukuru Mungu,” amesema Spika Ndugai.

Ambapo Bungeni Dodoma Spika Ndugai ameamua kutumia dakika chache kueleza sifa na kazi zilizofanywa na Dk. Mengi katika uhai wake kwa manufaa ya taifa miongoni mwa hayo ni uchangiaji wa kiasi cha Sh. 50 milioni katika mradi wa kujenga vyoo kwa watoto wa kike katika majimbo yote Tanzania.

Bunge litaukumbuka mchango wa Dk. Mengi enzi za uhai wake, ikiwemo kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi kupitia sekta ya viwanda na tasnia ya habari, pia alikuwa mstari wa mbele katika kusaidia shughuli za ulinzi wa mazingira, pamoja na kusaidia watu wasiojiweza na wenye uhitaji.

“Tunamshukuru Dk. Mengi kwa mchango wake mkubwa usiopimika katika taifa hili, tutamkumbuka daima kwa jinsi alivyosaidia sana hifadhi ya mazingira hasa maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro kwa mamilioni bila kuchoka, alikuwa mmiliki wa vyombo vya habari na mmiliki wa viwanda kadhaa,” amesema Spika Ndugai na kuongeza;

“Na alikuwa kiongozi wa umma akiwa ni mwenyekiti wa bodi mbalimbali na mengine mengi ya binafsi. Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mazingira na Kamishna wa TACAIDS.”

Spika Ndugai amesema, katika maisha yake Dk.  Mengi alipata tuzo nyingi za kitaifa na kimataifa, alijulikana kwa utoaji misaada ya kijamii, ujenzi wa misikiti, makanisa.

Pia alikuwa msaada kwa wasiojiweza ikiwemo walemavu wanyonge na kutoa tiba kwa wagonjwa mbalimbali hasa wa moyo.

Ujumbe wa mwisho Mengi alioandika kwa mke wake na Watanzania
Mengi umekwenda wapi?, JPM ampa Lukuvi maagizo mazito