Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa mhimili huo umesitisha kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad hadi atakapofika mbele ya Kamati ya Bunge kama alivyoelekeza.

Spika Ndugai ambaye amepangua wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), amesema kuwa pamoja na kufanya mabadiliko hayo, amesitisha kazi za kamati hizo hadi pale CAG atakapofika mbele ya Kamati ya Bunge Januari 21 mwaka huu.

Kiongozi huyo wa Bunge amesema kuwa wamesikitishwa na kauli ya CAG kuliita Bunge hilo kuwa ni dhaifu, na kwamba wamelichukulia suala hilo kwa umakini mkubwa tofauti na baadhi ya wanasiasa wa upinzani wanavyolizungumzia.

“Hili jambo sio la utani utani kama hao kina Zitto (Mbunge wa Kigoma Mjini) wanavyocheza huko Dar es Salaam, sisi hili jambo lililotokea limetusikitisha sana kiukweli. Huwezi kutuita sisi dhaifu halafu wewe ni mtu unatakiwa kufanya kazi na sisi,” Mtanzania wanamkariri Ndugai.

“Sisi hatutegemei utuite dhaifu yaani kama mazezeta, hiyo ni kuonyesha kwamba si kwamba tumevunja hizo kamati. Ila kwa sasa tumesitisha kazi ya hizo kamati kwa muda. Kwa hiyo wabunge kama wabunge watafanya kazi kupitia kamati nyingine,” aliongeza.

“Tumesitisha kwa muda ili hili jambo la huyu ambaye ni mshirika wetu (CAG- Profesa Assad) katika kufanya kazi, kwanza afike mbele ya Kamati ya Bunge aeleze kama sisi ni wadhaifu ama laa. Vinginevyo hatuna haja ya kufanya naye kazi ili atafute hao ambao ni ‘strong’ (wenye nguvu) afanye nao kazi,” Mtanzania wanaendelea kumkariri Ndugai.

CAG alitoa kauli hiyo alipokuwa akifanya mahojiano na kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, ambapo alieleza kuwa Bunge kutofanyia kazi kikamilifu Ripoti anazoziwasilisha ni ‘udhaifu wa Bunge’.

Kutokana na kauli hiyo, Spika wa Bunge alimtaka CAG kufika katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kujieleza.

Maadhimisho mengine ya kitaifa yafutwa
Shahidi: Bilionea wa Unga ‘El Chapo’ alimhonga Rais wa Mexico