Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Athuman Kihamia hakuwa sehemu ya ufisadi wa Sh3.5 bilioni zilizopigwa na baadhi ya vigogo wa Halmashauri ya Kaliua.

Hayo yamebainika leo bungeni jijini Dodoma kupitia kwa mbunge wa viti maalum (CCM), Amina Mollel alipokuwa akitoa taarifa kwa lengo la kuweka sawa kumbukumbu dhidi ya hoja aliyoitoa Mbunge wa viti maalum, Tunza Malapo (Chadema) na kutaja jina la Kihamia.

Katika hoja yake, Malapo ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alisema kuwa ukaguzi wa kamati hiyo uliobaini ufisadi huo ulifanywa kati ya Mwaka wa Fedha 2012/13 na 2016/17, na kwamba Kihamia ni mmoja wa waliokuwa Wakurugenzi katika kipindi hicho.

Katika taarifa yake dhidi ya hoja ya Malapo, Mollel alisema kuwa Mkurugenzi Kihamia aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kaliua Januari 2015 wakati mkataba uliobainika kuwa na ufisadi uliingiwa mwaka 2014.

Alifafanua kuwa baada ya kuteuliwa, Kihamia ndiye aliyebaini ufisadi huo na kutoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa wakati huo ili achukua hatua sitahiki.

“Niweke tu kumbukumbu sahihi kwamba Mkurugenzi, Athumani Kihamia aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Kaliua Januari 2015, na wakati huo anateuliwa tayari mikataba ilikuwa imeshaingiwa mwaka 2014,” alisema Mollel.

“Kwahiyo mheshimiwa Spika, Athuman Kihamia ndiye aliyetoa hizo taaria. Na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa wakati huo akatuma Tume kwa ajili ya kwenda kufuatilia. Kwahiyo hahusiki na hizo tuhuma,” aliongeza.

Baada ya ufafanuzi wa Naibu Spika, Dkt. Tulia Ackson kuhusu kanuni za Bunge zinazokataza kutoa taarifa za uongo, Malapo alionesha kutopinga ufafanuzi huo na kusimamia hoja yake kuwa Mkurugenzi huyo alihudumu katika kipindi ambacho ukaguzi ulifanyika.

Katika ripoti ya LAAC pamoja na Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), ufisadi wa takribani Sh31 bilioni za fedha za umma ulibainika.

Awali, akizungumzia ufisadi wa Sh3.5 bilioni katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, Mwenyekiti wa LAAC, Vedasto Ngombale alisema Mkuu wa Mkoa wa wakati huo, Fatma Mwassa alitumia madaraka yake vibaya kuingilia mchakato wa zabuni na kulazimisha apewe mkandarasi wa kampuni ya Saram ambaye ana uhusiano naye wa ndani.

“Mkuu wa mkoa wa wakati huo alimuelekeza mkurugenzi, wenyeviti wa kamati za tathmini, bodi ya zabuni na mkuu wa kitengo cha ununuzi kutoa zabuni kwa kampuni hiyo ambayo mkurugenzi wake ni mtu mwenye uhusiano wa ndani na Mwassa,” alisema Ngombale.

Kamati hiyo imependekeza wote waliohusika watafutwe na kuchukuliwa hatua kwa matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa fedha za umma.

Video: Wanawake Vinara mtandao wizi wa Bodaboda
Emery amvulia kofia Pep Guardiola kabla ya Man City Vs Arsenal

Comments

comments