Hatimaye, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anaweza kupata dhamana baada ya Jaji wa Mahakama Kuu, Dk Modesta Opiyo kuwapa muda wa siku 10 mawakili wa mbunge huyo kukata rufaa ya kuomba dhamana.

Akitoa uamuzi huo jana, Jaji Opiyo alieleza kuwa Mahakama haioni sababu za kuendelea kuzuia kuongezewa kwa muda wa kukata rufaa ya kuomba dhamana ambayo ni haki ya kila mtuhumiwa na kwamba suala hilo linahitaji busara kuamua.

“Mahakama haina sababu ya kuzuia haki isitekelezeke kwa kuzuia uongezaji wa muda kama kuna ucheleweshaji usiokuwa wa kawaida,”

“Mahakama inaruhusu maombi haya na kumpa siku kumi ya kuonyesha nia ya kukata rufaa,” aliongeza.

Kupitia kesi hiyo inayovuta umati wa watu wengi, Lema anashtakiwa kwa kosa la kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli katika mikutano yake aliyoifanya kwa nyakati tofauti jijini Arusha.

Lema amekuwa mahabusu tangu Novemba 2 mwaka huu alipokamatwa kwa tuhuma hizo alipokuwa mjini Dodoma na kusafirishwa hadi jijini Arusha. Kwa muda wote juhudi za mawakili wake kumtafutia dhamana ziligonga mwamba kutokana na kuwepo pingamizi la upande wa Jamhuri.

Magunia 102 ya 'Mchele wa Plastiki' yakamatwa Nigeria
Video: Lema aanza kuuona moshi mweupe, Mabaki ya Faru John utata mtupu...