Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi. Anthony Sanga na Mkurugenzi wa Kampuni ya Bennet Contractors, Sabato Boaz wamesaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa Maji wa Nyashimo wilayani Busega utakaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.8.

Mkataba wa Mradi huo utakaonufaisha vijiji vya Bukabile, Mwagulanja na Bulima na kuhudumia wananchi 20,030, umesainiwa Nyashimo wilayani Busega na kushuhudiwa na wananchi, viongozi wa Chama na Serikali wa Wilaya ya Busega na Mkoa wa Simiyu, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka.

Akizungumza na wananchi na viongozi waliofika kushuhudia zoezi hilo Mtaka amemtaka Mkandarasi Kampuni ya  Bennet Contractors kuzingatia muda na viwango katika utekelezaji wa mradi huo, huku akisisitiza kuhakikisha mradi huo unawanufaisha wananchi wanaozunguka eneo la mradi kwa kutoa ajira za muda na ununuzi wa vifaa vya ujenzi.

“Mkataba unaonesha mradi huu ni wa miezi 15, nikuombe mkandarasi miezi 15ni mingi tungehitaji tunapoanza maandalizi ya kutengeneza ilani ya CCM mwaka 2020 tuzungumzie utekelezaji wa ilani siyo mpango; tunahitaji jamii yetu inufaike kupitia mradi huu, vijana wapate ajira, mama ntilie wapike chakula na baadhi ya vifaa vya ujenzi vinunuliwe kwenye maduka ya hapa,”amesema Mtaka.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 16.4  kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maji wilayani Busega, ikiwa ni pamoja na Mradi wa Lamadi, Kiloleli, Mwamanyili na ukarabati wa visima maeneo mbalimbali, ambayo itakapokamilika  itaongeza hali ya upatikanaji wa maji safi na salama Busega kutoka asilimia 39 ya sasa na kufikia asilimia 74.

Kwa upande wake Mbunge wa Busega, Dkt. Raphael Chegeni amesema pamoja na mradi wa Nyashimo Serikali inatekeleza miradi mingine ya maji wilayani Busega ukiwepo wa Kiloleri Mradi wa Lamadi, hivyo akasisitiza wananchi kulinda na kutunza miradi hiyo ili iwanufaishe.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Bennet Contractors(Mkandarasi) Sabato Boaz kutoka Mwanza, amesema pamoja na kwamba mkataba unaonesha utekelezaji ni miezi 15, kampuni yake inatarajia kutekeleza kwa ubora na kwa muda mfupi kadri itakavyowezekana ili kuleta  huduma ya maji safi na salama haraka kwa wananchi wa Nyashimo.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC yaonya kuhusu taarifa za kizushi
Keisha awashukia wanaokosoa Dkt Bashiru kumuombea Makonda msamaha