Shirikisho la soka barani Afrika CAF limesisitiza kuwa makini na suala la viwanja vitakavyotumika katika fainali za AFCON kuanza mwaka 2019, ili kutoa ushindani sahihi kwa mataifa shiriki.

CAF wametangaza suala hilo, kufuatia mlalamiko ya baadhi ya makocha wa timu za taifa zilizoshiriki fainali za Afrika za mwaka huu 2017, ambapo walidai baadhi ya viwanja vilivyotumika vilikua na kiwango duni.

Kocha wa Ghana Avram Grant aliongoza malalamiko ya makocha wengine wa timu shiriki, kwa kudai ilikua ni rahisi kwa wachezaji kupata majeraha kutokana na viwanja vilivyotumika, hususan katika sehemu ya kuchezea.

Grant alisema ilikua ni vigumu kwa kila mmoja kuamini kama Gabon walikua makini kwenye maandalizi ya viwanja vyao vilivyotumika kwa ajili ya fainali za mwaka 2017.

Katibu mkuu wa CAF Hicham El Amrani amesema, watakua makini katika kuhakikisha viwanja vitakavyotumika katika fainali zijazo vinakua katika ubora wa hali ya juu, ili kuepusha malalamiko yasiyo na lazima.

Amesema waliyasikia malalamiko kutoka kwa baadhi ya makocha ambao walihofia wachezaji wao kuumia kutokana na sehemu za kuchezea kuwa katika kiwango duni, hivyo hawana budi kufanya litakalowezekana ili kuepusha kadhia hiyo.

Agizo la kuhakikisha viwanja vinakua na sehemu nzuri ya kuchezea, linaelekezwa moja kwa moja kwa taifa la Cameroon ambalo litakua mwenyeji wa fainali zijazo za mwaka 2019.

Video: Mbunge Lissu aligawa Bunge, Makonda akamiwa
Mpango: Hali ya uchumi ni mbaya kusini mwa jangwa la sahara