Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’ imefanya mabadiliko ya Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ‘2022/23’ kwa mara nyingine, ili kuzipa nafasi klabu za Simba SC, Young Africans na Azam FC zinazoshiriki Michuano ya Kimataifa.

Miamba hiyo mitatu ya Dar es salaam mwishoni mwa juma lijalo itacheza michezo ya Mzunguuko wa Kwanza ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Taarifa iliyotolewa na ‘TPLB’ leo Ijumaa (Septemba 30) mchana imeeleza kuwa, mchezo namba 53 kati ya Simba SC dhidi ya Singida Big Stars uliokuwa umepangwa kuchezwa Oktoba 12 katika Uwanja wa Liti mkoani Singida, umeahirishwa na utapangiwa tarehe nyingine.

Mchezo namba 54 kati ya Azam FC dhidi ya Dodoma jiji FC uliokuwa umepangwa kufanyika Oktoba 12 katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam, umeahirishwa na utapangiwa tarehe nyingine.

Mchezo namba 56 wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans dhidi ya Namungo FC uliokuwa umepangwa kuchezwa Oktoba 13 kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, nao umeahirishwa na utapangiwa tarehe nyingine.

Ikumbukwe kuwa Simba SC itacheza dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Angola Premero de Agosto, ikianzia ugenini kati ya Oktoba 09, kisha itamalizia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Oktoba 16.

Azam FC wao watakipiga dhidi ya Al Akhdar ya Libya katika Michuano ya Kombe la Shirikisho, wakianzia ugenini Oktoba 08, na baadaye watacheza mchezo wa Mkondo wa Pili nyumbani Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam kati ya Oktoba 14-16.

Young Africans wao wataanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Oktoba 08, wakicheza dhidi ya Mabingwa wa Sudan Al Hilal na baadae Oktoba 16 watakuwa ugenini mjini Kharoum-Sudan kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili

Simba SC yaita mashabiki kwa Mkapa
Safari zisizo lazima zisitishwe kuepuka Ebola