Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limezipa kampuni mbili haki ya kurusha moja kwa moja ya mechi ya Kundi G kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kati ya wenyeji, Tanzania dhidi ya Misri kesho.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, Televisheni hizo ni Azam TV ya Tanzania na Bein TV ya Cameroon.

Azam TV watarusha mchezo huo kupitia chaneli ya ZBC 2, wakati Bein wataonyesha kupitia beIN SPORTS na beIN SPORTS 2.

Taifa Stars inatarajiwa kumenyana na Misri kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Kundi G kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Katika mchezo wa kesho, Stars inahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kwenda AFCON ya mwakani.
Tanzania inashika mkia katika Kundi G, baada ya kucheza mechi mbili, ikifungwa moja ugenini na Misri 3-0 na kutoa sare moja ya 0-0 na Nigeria nyumbani.

Misri inaongoza kundi hilo kwa pointi zake saba baada ya kucheza mechi tatu sawa na Nigeria yenye pointi mbili.
Zote, Misri na Nigeria zimebakiza mchezo mmoja mmoja, wakati Tanzania ina mechi mbili – kwanza Jumamosi na Misri nyumbani na baadaye Septemba na Nigeria ugenini.

Iwapo Tanzania itashinda mechi zote mbili za mwisho watamaliza na pointi saba sawa na Misri, hivyo timu ya kufuzu AFCON ya mwakani kutoka Kundi G kupatikana kwa wastani wa mabao.

Habari Mpasuko: Muhammad Ali afariki
Polisi waitosa ahadi waliyompa Maalim Seif, alalama