Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amemuagiza Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG), kuufanyia uchunguzi mfuko wa kuendeleza zao la Korosho uliokuwa na kiasi cha shilingi bilioni 53.2 ambazo zingetumika kujenga maghala na viwanda vitatu vya kubangua korosho baada ya kubaini kuwepo na udanganyifu.

Hasunga ameyasema hayo jijini Dodoma Novemba 17, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa Habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo ambapo pia ameunda timu ya watu watano kwa ajili ya kuhakiki kiasi cha korosho kilichopokelewa na kilichouzwa katika msimu wa Korosho wa mwaka 2018/2019.

“Kamati za ulinzi na usalama naziagiza kusimamia zoezi la uhakiki ambalo linaonekana kutawaliwa na udanganyifu hivyo timu iliyoundwa itashirikiana na timu iliyokuwepo chini ya wizara Kilimo kuhakiki pia fedha zilizopatikana ili kuhakikisha wanaolipwa ni wale wanaostahili,” amebainisha Hasunga.

Amesema timu hiyo inatakiwa kuhakikisha kama ni kweli majina yaliyotoka kwenye vyama vya msingi kwenda vyama vikuu na kiasi cha fedha zilizoingizwa benki kwenye akaunti za wakulima na endapo kuna udanganyiufu uliojitokeza waoneshe ni kwa kiwango gani ili kusaidia serikali kutoa taarifa ya uhakika.

Aidha waziri Hasunga amesema mwaka 2016 serikali iliamua kufuta mfuko wa wakfu uliokuwa na kiasi cha fedha shilingi bilioni 53.2 kwenye akaunti lakini bodi ya korosho nchini (CBT), iliamua kubadili matumizi ya fedha hizo tofauti na maagizo ya serikali.

“Sisi wizara hatupo tayari kuona ubadhilifu wowote wa fedha za umma unafanyika maana Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli haipo tayari kukubali kuona watu wachache wanafaidika na fedha za walipa kodi za watanzania,” ameongeza Hasunga.

Hata hivyo ametoa msisitizo kwa timu zote mbili alizoziunda kuhakikisha hadi kufikia Januari 15, 2020 ziwe zimeshakamilisha na kuletea ripoti Wizarani na kuwahakikishia kuwa Serikali haitomvumilia yeyote mwenye kutaka kuzigusa fedha za wananchi.

Aidha waziri huyo ambaye aliambatana na naibu wake Hussein Bashe katika kikao hicho amesema CBT ilionesha kutumia kiasi cha shilingi bilioni 28.1 kununua viuatilifu na shilingi bilioni 12.2 kulipia magunia wakati uhalisia ni kuwa katika msimu huo wanunuzi walinunua magunia wao wenyewe.

Kufuatia hali hiyo waziri Hasunga ametoa wito kwa wakulima kuwa endapo kuna yeyote anayedai katika vyama vya ushirika kupeleka madai yake kwa kamati ya ulinzi na usalama na timu iliyoundwa ili aweze kushughulikiwa stahiki zake.

LIVE: Yanayojiri katika Mkutano wa Makonda na Viongozi wa dini zote
Video: Mkapa atoboa siri ya Magufuli, Serikali kumsaidia mtoto aliyefiwa wazazi, ndugu