Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amesema kuwa Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (RBT) una mapungufu ya magari 165.

Ripoti ya CAG ya mwaka 2017/18 imeeleza kuwa mradi huo ulipaswa kuwa na jumla ya mabasi 305 katika awamu yake ya kwanza.

Ameeleza kuwa upungufu huo wa mabasi umesababisha mabasi kujaa kupita kiasi kilichopangwa, hali inayosababisha uchakavu na uharibifu wa haraka wa mabasi hayo.

“Upungufu huo wa mabasi umesababisha ucheleweshwaji wa usafiri kwa wananchi, abiria kujaa kupita kiasi kwenye mabasi hayo,” ameeleza CAG.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa Usafiri Dar es Salaam Rapid Transit (Udart) ilijiendesha kwa hasara ya Sh. 6.78 bilioni katika miezi nane ya awamu yake ya kwanza iliyoanza Mei 10, 2016.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hasara hiyo ilitokana na matumizi ya Sh26.57 bilioni kwa kulinganisha na mapato ya 19.78 bilioni.

Aidha, imeeleza kuwa matumizi mengine yalikuwa na shaka. Alisema kuwa ingawa Udart iliripoti kutumia Sh. 6.02 bilioni kwa ajili ya mafuta, vitabu vya mahesabu vilionesha kuwa mafuta yaliyotumika yana thamani ya Sh.4.79 bilioni tu.

“Ninapendekeza kuwa Udart iongeze idadi ya mabasi yake ili kukidhi mahitaji ya sasa na kuboresha utoaji wa huduma,” inaeleza ripoti ya CAG.

Aidha, amependekeza kuwa mahesabu ya Udart yapitiwe upya na kiasi cha Sh.508.31 milioni ambacho hakionekani kiweze kurejeshwa na watu waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Mkuu wa usalama amehaidi kukabiliana na uchochezi nchini
Kim Jong Un ampa Trump masharti ili kukutana naye tena

Comments

comments