Aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoh amejaribu kutegua kitendawili cha uhalali wa Spika wa Bunge, Job Ndugai kumtaka CAG, Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Bunge Januari 21 vinginevyo atafikishwa kwa pingu.

Spika Ndugai alitoa maelekezo hayo wiki hii kutokana na kile alichokieleza kuwa Profesa Assad alilidhalilisha Bunge kwa kudai kuwa ni dhaifu alipofanya mahojiano na kituo cha habari akiwa nchini Marekani.

Akijaribu kutegua kitendawili hicho ambacho kimeibua gumzo kubwa la kisheria hususan kuhusu kinga ya CAG, Utoh ameeleza kuwa taasisi hizo mbili zinapaswa kuelewana.

Amesema kuwa kitendo cha CAG kukutana na Spika wa Bunge ni suala la kawaida katika utendaji wao lakini kitendawili kinachobaki ni namna inayotumika kumuita.

“Spika kukutana na CAG ni suala la kawaida, lakini it’s a manner (ni namna) iliyofanyika. Unajua CAG analindwa sana na Katiba lakini Spika naye anasema kanuni za Bunge zinamruhusu, sasa hapo litakuwa suala la kisheria,” Mwananchi inamkariri Utoh.

Akiongea na waandishi wa habari wiki hii, Spika Ndugai alieleza kusikitishwa na kauli ya CAG dhidi ya Bunge. Alieleza kuwa Bunge ambalo ni wawakilishi wa wananchi ndio Bosi wa CAG na ndio sababu anawasilisha ripoti yake kwa Bunge hilo, hivyo anapaswa kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Aidha, Spika Ndugai alieleza kuwa ingawa Katiba inampa kinga CAG kama taasisi huru, bado ana wajibika kwa Bunge na hawezi kuwa huru kufanya atakavyo.

Hatua hiyo imeibua mijadala mingi yenye maoni tofauti. Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameeleza kuwa wamekubaliana na baadhi ya wabunge wa Upinzani kuliwasilisha suala hilo Mahakamani ili kupata ufafanuzi wa Kikatiba kuhusu kinga ya CAG.

Mpinzani atamba kushinda Urais DRC, Marekani yatuma jeshi
Marehemu aliyezikwa miezi mitano iliyopita afukuliwa