Bingwa wa dunia wa masumbwi ya uzito wa kati, Saul Alvarez maarufu kama Canelo usiku wa leo atatetea ubingwa wake dhidi ya bondia hatari, Daniel Jacobs.

Wababe hao wawili watapigana kwenye ukumbi maarufu wa GMG Grande jijini Las Vegas nchini Marekani, katika pambano ambalo limevuta usikivu wa wapenzi wengi wa ndondi duniani kote.

Canelo na Jacobs wote wameshapambana na Gennady Golovkin aka ‘GGG’, na wote walimpa wakati mgumu bondia huyo ambaye alikuwa na rekodi ya kushinda kwa KO tupu, hali iliyovuta kiu ya wapenzi wa ndondi kutaka wao wawili pia wapimane misuli ulingoni.

Jana, katika tukio la kupima uzito, walishindwa kuvumiliana na kutaka kuzichapa kavukavu lakini watu wao wa karibu waliwaachanisha.

Canelo mwenye umri wa miaka 28 ambaye ni raia wa Mexico mwenye rekodi ya kushindwa pambano moja tu dhidi ya Floyd Mayweather mwaka 2013, ametamba kuwa baada ya kukutana na Jacobs ameona ana hofu dhidi yake hivyo atammaliza.

“Niliona hofu ndani yake na ndivyo alivyo hivi sasa. Kwangu mimi na watu wangu pamoja na mashabiki wangu, sisi ushindi ni jambo la muhimu zaidi,” alisema Canelo.

Kwa upande wa Jacobs, ni bondia mzoefu, mwenye kasi na nguvu ambaye amewahi kushindwa mapambano mawili tu ikiwa ni dhidi ya Golovkin na Dmitry Pirog. Lakini amekuwa bondia mgumu kupigika akikumbuka historia yake ya kushinda ugonjwa wa saratani aliowahi kuwa nao. Sasa anaamini hakuna cha kupoteza kirahisi.

“Sijawahi kurudi nyuma kutokana na changamoto yoyote ya maisha. Ninatokea Brownsville, Brooklyn, siwezi na haitawahi kutokea,” alisema Jacobs.

“Hii ni fursa ya maisha yangu na kwa sasa najisikia kama mimi ndiye bondia bora zaidi wa uzito wa kati duniani. Yule mjinga pale amenisukuma, nitajibu kwa ngumi yangu Jumamosi,” alisema Jacobs.

Canelo ni bondia ambaye ana jina kubwa na miaka ya hivi karibuni aliwahi kusaini mkataba uliomfanya kuwa mwanamichezo tajiri zaidi duniani mwaka huu kwa ambao hawajastaafu, baada ya kusaini dili ya £275milioni lakini mwaka jana rekodi yake ilivunjwa na mchezaji wa Baseball Mike Trout.

‘Dkt. Mwaka’ aeleza alivyofanya mazingaombwe hadi kuwa Tabibu
Video: Fahamu wanyama 5 tajiri zaidi duniani

Comments

comments