Aliyekuwa nahodha wa Taifa Stars Nadir Haroub ‘Cannavaro’ leo amepeleka barua TFF ya kutangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Tanzania kutokana kunyang’anywa unahodha bila utaratibu maalum na kupewa nyota wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta.

Cannavaro amesema, hakukuwa na tatizo kumpa unahodha Mbwana Samatta kwasababu anastahili kuwa nahodha wa kikosi cha taifa lakini amelalamikia utaratibu uliotumika kumvua unahodha huo na kumpa Samatta.

Amedai kuwa, hakupewa taarifa rasmi zaidi ya kuona kwenye TV na vyombo vingine vya habari kuwa amevuliwa unahodha na kupewa mtu mwingine. Cannaro ameongeza kuwa watangulizi wake Salumu Swed na Shadrack Nsajigwa waliagwa kwa heshima lakini yeye hajapewa taarifa rasmi hivyo anaona amedharauliwa.

Beki huyo kisiki wa klabu ya Yanga amesema, alikuwa bado anauwezo wa kuitumikia Stars kwa miaka mingine minne ijayo lakini ameamua kustaafu kutokana na kudhalilishwa kwa kuvuliwa unahodha kwenye vyombo vya habari.

“Nilikuwa na uwezo wa kucheza hata miaka mingine minne inayokuja kulitumikia taifa langu. Naipenda nchi yangu mimi ni mzalendo halisi, nimelitumikia taifa hili kwa miaka 10 na nilikuwa na nia ya kulitumikia kwa miaka mingine minne mbele lakini kitendo kilichofanywa cha kunivua unahodha kwenye TV kimenidhalilisha”, amesema Cannavaro.

“Sikuona kuthaminiwa, jitihada zangu zote za kujitolea kwa taifa hili hazikuthaminiwa. Mimi na Samatta ni marafiki, Samatta ni rafikiyangu sana na anastahili kuwa nahodha wa national team”.

“Kocha Boniface Mkwasa mimi namkubali sana tangu tukiwa Yanga, ni mtu ambaye hatujawahi kukwaruzana”.

“Mimi sijajiuzulu kwa kukasirika kutokana na kuvuliwa unahodha au Mbwana Samatta kupewa unaodha, kilichoniudhi mimi ni utaratibu uliotumika kunivua unahodha. Sikutegemea kuona navuliwa unahodha nikiwa nimekaa kwenye TV naangalia mechi ya Simba dhidi ya Mtibwa ya michuano ya Mapinduzi Cup”.

“Ilitakiwa kocha anipigie simu anitaarifu tukae chini nipewa taarifa na mimi nikubali. Salumu Swed alikuwa nahodha wa timu ya taifa alipostaafu tulimuaga Mwanza. Shadrack Nsajigwa ambaye mimi nimechukua mikoba kwake aliagwa vizuri na kwa amani kabisa lakini mimi nimedharaulika”.

Siku tatu baada ya Samatta kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za Afrika, kocha mkuu wa Taifa Stars Boniface Mkwasa alimtangaza rasmi Samatta kuwa ndiye nahodha mpya wa timu ya taifa ya Tanzania huku Cannavaro akipewa majukumu ya kuwa nahodha wa kikosi cha taifa kinachoshiriki CHAN lakini  Mkwasa akasema wanamtafutia nafasi nyingine kwenye kikosi cha Stars.

Mkwasa alimtangaza Samatta kuwa nahodha Stars wakati akiwa visiwani Zanzibar akifatilia michuano ya Mapinduzi Cup iliyomalizika juma lililopita.

Djokovic Ajitetea Tuhuma Za Kupanga Matokeo
Tuhuma Za Upangaji Wa Matokeo Kwenye Tennis