Kiungo wa Real Madrid Carlos Henrique José Francisco Venâncio Casimiro, atakuwa sehemu ya kikosi cha Zinedine Zidane kitakachoshuka dimbani hii leo kupambana na Cultural Leonesa katika mchezo wa kombe la Mfalme (King’s Cup).

Kiungo huyo kutoka nchini Brazil atakua akicheza kwa mara ya kwanza tangu mwezi Septemba, ambapo alivunjika mguu katika mchezo wa La Liga dhidi ya Villareal.

Kikosi cha Zidane kitahitaji kuendelea kutunza heshima ya kutokufungwa katika michezo 31, na katika mpambano wa mkondo wa kwanza dhidi ya klabu ya Cultural Leonesa inayoshiriki ligi daraja la kwanza, Real Madrid waliibuka na ushindi wa mabao 7-1.

“Mipango mikubwa kwa mchezo huo ni kumtumia Casemiro. Utakua mchezo wa kwanza kwake tangu alipopata majeraha ya kuvunjika mguu, na baada ya mchezo huo tutaangalia kama ataweza kucheza jumamosi,” Alisema Zidane katika mkutano na waandishi wa habari.

Katika hatua nyingine Zidane amesema mshambuliaji Cristiano Ronaldo hatokuwa sehemu ya kikosi chake hii leo, kutokana na kuhutaji kumpumzisha kwa lengo la kumtumia kwenye mpambano wa El Clasico.

Mshambuliaji huyo kutoka nchini Ureno, anaongoza kwa kupachika mabao katika ligi kuu ya Hispania (La Liga), kwa kufunga mara 10 mpaka sasa, ikiwa ni zaidi ya bao moja dhidi ya hasimu wake kisoka Lionel Messi.

Bastian Schweinsteiger Akumbukwa Old Trafford
Andres Iniesta Aongeza Matumaini FC Barcelona