Shirikisho la soka nchini Brazil CBF limethibitisha kusaini mkataba mpya na kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo Adenor Leonardo Bacchi Tite ambao utafikia kikomo mwaka 2022 mara baada ya fainali za kombe la dunia zitakazounguruma Qatar.

CBF wametangaza kusaini kwa mkataba huo, huku wakimpa majukumu mazito kocha Tite ya kuhakikisha kikosi cha Brazil kinafikia malengo kwenye michuano yote, watakayoshiriki katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Brazil itashiriki michuano ya kombe la mataifa ya kusini mwa Amerika (Copa America) mwaka 2019, na nchi hiyo itakua mwenyeji wa fainali hizo.

Kama wataibuka mabingwa wa michuano ya Copa America, Brazil watashiriki michauno ya kombe la mabara itakayofanyika nchini Qatar mwaka 2021.

Baadae timu ya taifa hilo itaanza mchakato wa kusaka nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia mwaka 2022 kupitia ukanda wa Amerika ya kusini CONMEBOL.

Kwa mara ya mwisho Brazil ilifikia lengo la kutwaa ubingwa mwaka 2013, baada ya kutawazwa kuwa bingwa wa michuano ya kombe la mabara iliyofanyika nchini kwao.

Kwa upande wa fainali za kombe la dunia, kwa mara ya mwisho Brazil ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo mwaka 2002 ilipochezwa katika nchi za Japan na Korea Kusini.

Mwaka 2007, ilikua mara ya mwisho kwa Brazil kutwaa ubingwa wa michuano ya kombe la mataifa ya Amerika ya kusini (Copa America), baada ya kuifunga Argentina mabao matatu kwa sifuri.

Tite alikua anapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa kombe la dunia mwaka huu 2018, lakini hakufanikiwa kutokana na kikosi chake kuondolea katika hatua ya robo fainali, baada ya kufungwa mabao mawili kwa moja na Ubelgiji.

Lugola amtwisha zigo jingine Inspekta Sirro
Mohamed Salah amkuna Juergen Klopp

Comments

comments