Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demnokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Tundu Lissu amesema hakushindwa na wala CCM haikushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwani matokeo yaliyotolewa yalikuwa ni ya kupikwa.

Lissu ameyasema hayo wakati akifanya Mahojiano maalum na Dar24 Media jijini Dar es Salaam na kuongeza uthibitisho wa kaluli yake unatokana na kitendo cha Tume ya Uchaguzi nchini – NEC, kumtangaza mshindi pekee na si kutaja matokeo ya wagombea wote wa nafasi ya Urais.

Amesema, “Sheria yetu ya uchaguzi inasema hivi, uchaguzi ukishafanyika matokeo yakatangazwa inatakiwa yachapishwe kwenye Gazeti la Serikali jimbo kwa jimbo nchi nzima, na ukiingia kwenye tovuti ama ya ZEC au NEC lazima uyakute, lakini hayapo na yaliyopo ni ya Tarehe 5 Januari 2021.”

Tundu Lissu, wakati akifanya mahojiano na Mwandishi wa Dar24 Media nyumbani kwake jijijni Dar es Salaam.

“Maana yake ni kwamba hawana matokeo ya uchaguzi wa Rais walimtangaza Magufuli tu, ukiwauliza napataje hayo matokeo hakuna majibu kwasababu matokeo ni ya kupikwa na ushahidi ni huo, na kushindwa uchaguzi ni kutoa matokeo, onesha matokeo,” amesisitiza Lissu.

Hata hivyo, Lissu amekiri kuwa hakushinda uchaguzi akitaja sababu kuwa hakukuwa na uwazi katika matokeo na kusema, “hizo kura 1,933,000 wanazosema CHADEMA ilipata ni za kutunga kwasababu hazina ushahidi wowote hata za mshindi pia hazina ushahidi.”

Kuhusu katazo la mikutano ya vyama vya siasa, na jinsi gani alipambana kama mwanasheria kuondoa katazo hilo Lissu amesema, mara kadhaa walishitaki mahakamani lakini ilishindikana na kwamba katazo hilo lilitokana na Serikali kuogopa kukosolewa na kusisitiza kuwa wajibu wa vyama vya upinzani ni kuikosoa Serikali.

Polisi yawasaka wezi wa vyakula na mali ajali ya Korogwe
Robertinho akubali uwezo wa Chama