Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, amesema CCM imefanikiwa kupita bila kupingwa katika nafasi za ugombea Wenye viti wa vijiji 6,248 kati ya vijiji 12,319 ambavyo ni sawa na asilimia 51 kutokana na kuwa chama pekee kilichochukua fomu za wagombea na kuzirejesha kwa nafasi hizo.

Amesema upande wa mitaa CCM imepita bila kupingwa mitaa 1,169 kati ya mitaa 4,263 sawa na asilimia 27 na pia kupita bila kupingwa kwenye vitongoji 37,505 kati ya vitongoji 64,384 ambavyo ni sawa na asilimia 58 kutokana na kutokuwa na chama kingine kilichochukua fomu katika maeneo hayo.

“Kwahiyo katika maeneo hayo na kwa nafasi nilizoziainisha wagombea wa CCM walikosa wenzao kwa ajili ya mchuano wa kuwania kupigiwa kura kwenye uchaguzi wa Serikaliza mitaa nchini, vyama vya siasa vinatakiwa kuwa na utashi kutokana na taratibu zote kwenda kama zilivyopangwa,” amesisitiza Waziri Jafo.

Aidha amesema wagombea waliochukua fomu kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) walikuwa 412,872 sawa na asilimia 74 na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) 105,937 sawa na asilimia 19 na Chama cha Wananchi (CUF) 24,592 ambao ni sawa na asilimia 4.

Vyama vingine ni ACT-Wazalendo 8,526 sawa na asilimia 1.5, NCCR-Mageuzi 2,244 sawa na asilimia 0.4 na vyama vingine vyenye usajili wa kudumu ambavyo vilichukua fomu chini ya asilimia 0.1 kwa kila kimoja kwa wagombea wote.

“Vyama hivi vingine vyenye usajili wa kudumu wao walichukua fomu chini ya asilimia 0.1 maana yake utakuta waliochukua chama kimoja labda kina watu sita, saba au nane na wengine walifikisha watu mia mbili na ukiwajumlisha ndio unapata hiyo asilimia 0.1,” amebainisha Waziri Jafo.

Aidha Waziri huyo wa TAMISEMI amesema katika zoezi la kuchukua na kurejesha fomu kulikua na changamoto kwa wagombea wengi kufanya makosa mengi ya kikanuni yaliyopelekea wengi wao kutoteuliwa siku ya uteuzi Novemba 5, 2019.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni pamoja na baadhi ya wagombea kujidhamini wenyewe kitu ambacho ni kinyume cha kanuni, kushindwa kujaza fomu namba nne, kutofautiana kwa majina, kutojaza fomu kwa ukamilifu na kukosea umri.

“Kwa mfano kuna fomu moja ilikua inatembea mtandaoni mtu amejaza umri wake kuwa alizaliwa mwaka 2019 yapo makosa mengi ya aina tofauti ambayo ilikua ni kigezo cha kuwaengua sasa mtu kazaliwa 2019 ukiipitisha fomu kama hiyo ina maana mtu huyo anagombea vipi uchaguzi,” amehoji Jafo.

Hata hivyo Jafo amesema makosa mengi yaliyotendeka yamesababishwa na viongozi wa vyama vya siasa kushindwa kutimiza wajibu wao kwa kuwaelekeza vyema namna ya kujaza fomu hizo wagombea wanaowawakilisha na kwamba kwa mwaka huu waliandaa kanuni bora ambazo kila mtu alipaswa kuzifuata.

Amesema kanuni hizo ziligawiwa na kuwekwa katika mitandao na kwamba kutokana na hali hiyo walitangazia watu wenye malalamiko kuwasilisha pingamizi ama kukata rufaa kwa lengo la kutatua makosa mbalimbali ambayo yangefanywa na kamati.

Rais wa Bolivia ajiuzulu, Atangaza uchaguzi Mpya
Video: Ngoma bado mbichi, Jafo apindua meza 'Nongwa' Serikali za Mitaa