Kiongozi wa Chama Cha Kijamii (CCK), mchungaji Dkt Godfrey Malisa ametangaza nia ya kukishtaki Chama Cha Mapinduzi kwa kile alichodai kimevunja sheria ya uchaguzi kwa kuanza kampeni mapema.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dkt. Malisa alisema kuwa chama hicho kilianza kufanya kampeni mjini Dodoma na baadae jijini Dar es Salaam baada ya kumpata mgombea wa urais ambaye alifanya mkutano mkubwa na kutoa ahadi kwa wananchi, kitendo ambacho kinatafsiriwa kuwa ni kufanya kampeni.

Dkt. Malisa alisema kuwa tayari ameshaiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuitaka ikichukulie chama hicho hatua stahiki kwa kuanza kampeni kabla ya muda. Alisema kama NEC haitachukua hatua stahiki, CCK na vyama vingine vya upinzani vitapeleka malalamiko yao mahakamani.

“Nafikiri CCM wanachofanya, wanatafuta goli la mkono ambalo waliwaahidi watanzania hivi karibuni,” alisema Malisa.

Aliwataka NEC kuvitendea haki vyama vyote vya kisiasa nchini hasa katika masuala ya uchaguzi na kwamba CCM kuwa chama tawala hakiipi haki ya kukiuka sheria.

Katika hatua nyingine, Dkt Malisa alisema kuwa anashangazwa na jinsi ambavyo polisi wanavyoweka ulinzi mkali kwa mgombea urais wa CCM tofauti na wanavyofanya kwa wagombea wa vyama vingine.

“Polisi wanapaswa kutoa ulinzi kwa watanzania wote, kwa nini wamejikita zaidi kwa mtu mmoja tu wakati kuna wengine wengi? Wagombea wote wanapaswa kuangaiwa kwa usawa.”

Dkt Malisa anatarajiwa kuwa mgombea wa urais kupitia chama chake cha CCK.

Navio Atangaza Ujio Mpya Wa Kundi Lake Na Album
Makongoro Ajipanga Kumvaa Halima Mdee ‘Kawe’