Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mara kimesema kinaandaa utaratibu wa kumuita katika vikao na kumhoji aliyekuwa Waziri wa mambo ya ndani Kangi Lugola ili awaeleze sababu zilizopelekea kuaibisha mkoa huo na Rais John Magufuli ambaye alimuamini na kumpatia nafasi ya uwaziri ili atumikie Taifa.

Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Samuel Kiboye wakati akieleza namna ambavyo chama hicho kinakasirishwa na viongozi wanaopewa nafasi ya kumsaidia Rais katika wizara mbalimbali lakini mwisho wa siku wanaliingiza Taifa katika mikataba mibovu.

Mwenyekiti huyo amesema kitendo cha Lugola kukiuka sheria za uongozi kimewaletea doa wana Mara kwasababu hata mwasisi wa Taifa Hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake alikuwa mstari wa mbele kukataa na kukemea rushwa hivyo walitarajia kila kiongozi anayetoka mkoa huo kuwa muadilifu.

“Tunatarajia kila mtu anayepewa nafasi katika mkoa wa Mara kwaajili ya kuwatumikia Watanzania, kuwa mwadilifu, mzalendo na mpinga rushwa kwa nguvu zote, kwa hili Mheshimiwa Lugola ameuaibisha mkoa wa Mara, hivyo muda wowote tutamuita katika vikaovyetu ili ajieleze” amesema Kiboye.

Amesema mkoa wa Mara unaendelea kuwa alama kwa Taifa kutokana na umuhimu wake wa kumtoa mwasisi wa Taifa, hivyo heshima hiyo inapaswa kuendelea kudumishwa na watu wote wakiwemo viongozi kuanzia ngazi  ya kitongoji, kata, wilaya mkoa na hata Taifa.

“Ni wazi kuwa, hatukubali kushuhudia mtu ambaye kwa namna moja au nyingine matendo yake yana dhamira ya kudhoofisha juhudi za Serikali ya awamu ya tano ambazo zimeonesha njia kwa kila sekta”amesema Kiboye.

Kangi Lugola alitumbuliwa hivi karibuni akiwa jukwaani na Rais Magufuli wakati wa makabidhiano ya nyumba za jeshi la Magereza, ikiwa ni siku 572 tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.

Magufuli alisema viongozi wa wizara hiyo walitia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Trilioni 1 kutoka kampuni moja ya nje bila kufuata sheria.

 

Video: Historia fupi ya marehemu Doglas, mwandishi TBC, ''Mwili uligundulika siku ya nne, ulianza kutoa harufu''
ARV's zapunguza kasi ya saratani ya ngozi

Comments

comments