Siku chache baada ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) kueleza kuwa hawajapokea majibu kwa barua rasmi ya mualiko wa mdahalo wa wagombea urais kutoka kwa vyama vya CCM na Chadema, vyama hivyo vimepinga taarifa hizo kwa nyakati tofauti.

Juzi, mjumbe wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba alipinga maelezo ya MCT na kudai kuwa chama chake kilijibu na kukubali mualiko huo kwa barua iliyofikishwa kwenye ofisi za chama hicho.

Makamba pia alisisitiza kuwa Katibu Mkuu wa CCM alikaa na baadhi ya viongozi wa MCT na kujadiliana nao kuhusu mdahalo huo, taarifa ambazo zinatofautiana na zile zilizotolewa na baraza hilo kupitia vyombo vya habari.

Kwa upande wa Ukawa, mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia alisema kuwa bado hawajapata barua kutoka MCT kuhusu kushiriki mdahalo kama walivyoeleza.

“Bado hatujapata barua ya MCT kama walivyosema, nilienda hadi Makao Makuu ya Chadema kuuliza kwa sababu mgombea wetu ni wa Chadema, hakuna barua hiyo. NCCR-Mageuzi pia hakuna barua hiyo,” alisema Mbatia.

Aliongeza kuwa Baraza hilo lilipaswa kuwasilisha barua na kuwakutanisha wawakilishi wa pande zote kujadili mazingira na taratibu zote za mdahalo husika kabla ya mdahalo huo, kitu ambacho hakijafanyika.

Hivi karibuni, MCT waliwaambia waandishi wa habari kuwa ingawa walituma barua za mwaliko wa mdahalo kwa vyama vyote vilivyosimamisha wagombea urais lakini ni vyama viwili tu vilivyojibu huku CCM na Chadema wakiwa katika kundi la vyama ambavyo havikujibu.

 

Busungu Aomba Angalau Dakika 30
Mamia Ya Wahujaji Wafariki Kwa Kukanyangana Makka