Vuta nikuvute inayoendelea kisiwani Zanzibar kufuatia mgogoro wa uchaguzi uliotokana na tangazo la kufutwa kwa uchaguzi imezua jambo baada ya kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa CCM wameridhia mgombea wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad aapishwe kuwa rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai amefanya mkutano na waandishi wa habari na kukanusha vikali taarifa hizo.

Vuai ameeleza kuwa taarifa hizo ni za kutungwa na kwamba zimemsingizia kuwa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika sherehe za kuapishwa kwa Maalim Seif na kwamba Dk Ali Mohammed Shein amekubali kuwa Makamo wa Kwanza wa rais.

“Taarifa hizo zilinisingizia kuwa nimewataka wananchi waridhie Dk Ali Mohammed Shein kuwa Makamo wa kwanza wa rais mara baada ya kuapishwa kwa Maalim Seif,” alisema.

Aliongeza kuwa chama chake kimepanga kumfungulia mashtaka mtu aliyetunga taarifa hizo za uongo na kuzisambaza.

Akizungumzia mazungumzo yanayoendelea kati ya Maalim Seif na Dk Shein, Vuai alisema kuwa mazungumzo hayo hayatabadili sheria kwa kuwa uchaguzi umeshafutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali.

Hata hivyo alipongeza mazungumzo hayo yanayoendelea na kueleza kuwa yana lengo la kudumisha amani na kwamba chama chake kinaendelea kujiandaa na marudio ya uchaguzi.

Zitto Kabwe Adai Lowassa Aliwavuruga
Angalia Pogba Alivyoonyesha Kuguswa Na Shambulio La Paris