Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeitaka Serikali kutafuta kiini cha tatizo katika sakata la mgomo wa wafanyabiashara kariakoo na kutafuta ufumbuzi.

Maelekezo hayo yametolea katika kikao maalumu kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan baada ya kupokea na kujadili taarifa kuhusu mgogoro wa wafanyabiashara wa soko hilo la kimataifa.

“Kamati Kuu baada ya kujadili imeielekeza Serikali kufanya uchambuzi wa kina wa masuala yaliyoibuliwa na kulalamikiwa na wafanyabiashara wa Kariakoo ili kutafuta kiini cha tatizo halisi na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu,”imesema taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema.

Kadhalika, Kamati Kuu imeielekeza Serikali kuhakikisha inatengeneza utaratibu wa kutatua changamoto mapema kabla hazijaleta madhara katika jamii kama ilivyokuwa katika mgogoro wa soko la Kariakoo.

Ikiwa ni siku tano zimepita tangu wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wamalize mgomo wao ambao ulifanyika kwa siku tatu mfululizo kwa kufunga maduka yao kushinikiza kutolewa kwa kodi ya stoo na kukomeshwa kwa kile walichokiita kamatakamata inayofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Itakumbukwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya vikao viwili na wafanyabiashara hao ambapo kikao cha kwanza kilifanyika Mei 15, 2023 hakikumaliza mgomo huku baadhi ya wafanyabiashara wakiendelea na mgomo hivyo kulazimika tena Mei 17, 2023 kufanya kikao kingine cha wazi katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Katika kikao cha pili kilichohudhuriwa na mamia ya wafanyabiashara wa soko hilo maarufu nchini lenye kila aina ya pilikapilika kilifanikisha kumaliza mgogoro huo baada ya Majaliwa pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ashatu Kijaji kuwasikiliza wafanyabiashara hao wakitema nyongo kuhusu kero zinazowasibu na baadaye kuunda kamati ya watu 14 kushughulikia matatizo hayo ikiwahusisha wafanyabiashara na watumishi wa Serikali.

Serikali kuja na mpango maalum ufugaji wa Samaki
Mayele: Wachezaji Azam FC wanakamia mechi