Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimejibu hoja zilizotolewa jana na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alipotangaza kuanza kwa operesheni maalum waliyoiita Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA).

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, chama hicho kimeeleza kuwa tamko hilo la Chadema limejaa uongo, ghiliba na ubabaishaji.

Ole Sendeka amesema kuwa wapinzani wamekosa hoja ya kuzungumzia katika awamu hii kutokana na utendaji kazi mzuri wa Rais John Magufuli, hivyo wameona ni bora kutunga uongo.

Chadema walitangaza jana kuzindua Oparesheni waliyoiita UKUTA nchi nzima Septemba Mosi mwaka huu kwa kufanya mikutano na maandamano.

Mbowe aliwataka wanasheria wote wa chama hicho kukutana na mwanasheria mkuu wa chama, Tundu Lissu kwa ajili ya kufuatilia taratibu za kisheria za masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupinga mahakamani zuio la kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa nchini.

Waziri Mkuu akabidhiwa matawati kwaajili ya Shule za Dar
Rais Magufuli atengua uteuzi wa Dk, James bodi ya Barabara