Wakati mgogoro wa Uchaguzi wa Zanzibar ukiendelea kutafutiwa ufumbuzi, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeeleza kuwa kimejiaandaa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi wa marudio ambao kimedai hauepukiki.

Kamati maalum ya chama hicho jana ilifanya kikao chini ya uenyekiti wa Dk. Ali Mohamed Shein na kueleza kuridhishwa na hatua za mazungumzo ya kutafuta muafaka zinazofanywa kati ya mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Dk. Ali Mohamed Shein. Makamu wa rais, Bi. Samia Suluhu pia alihudhuria kikao hicho.

Akitoa taarifa ya kikao hicho kwa vyombo vya habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM upande wa Zanzibar, Waride Bakari Jabu aliwataka wanachama wa CCM visiwani humo kujiandaa kikamilifu na marudio ya uchaguzi na kutorubuniwa na propaganda zinazoenezwa kuwa hakutakuwa na marudio ya uchaguzi.

“Kikao kimewataka wana CCM kujiimarisha lakini pia kujiweka tayari na hatimaye kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio ambao tarehe yake itatajwa na Tume ya Uchaguzi. Haya yote yanafanyika ili kuweza kukiwezesha chama cha mapinduzi kiweze kushinda kwa kishindo,” alisema Waride Bakari Jabu.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alitangaza kuufuta uchaguzi wa Zanzibar kwa maelezo kuwa uligubikwa na kasoro nyingi. CUF inaamini kuwa imeshinda katika uchaguzi huo na imekuwa ikiitaka ZEC kukamilisha zoezi la uhakiki wa matokeo na kumtangaza mshindi.

Rais Magufuli awaapisha Mawaziri na Manaibu Waziri Waliokuwa Wamesalia
BEN POL AELEZA KILICHOPELEKEA ‘AVRIL’ KUTOONEKANA KWENYE VIDEO YA 'NINGEFANYAJE