Sakata la mauaji ya mwandishi wa habari wa gazeti la Washington Post, Jamal Khashoggi limechukua sura mpya baada ya CCTV kamera kuwaumbua baadhi ya makachero wa ubalozi wa Saudi Arabia nchini Uturuki.

Uchunguzi wa picha za CCTV kamera uliofanywa na vyombo vya usalama vya Uturuki, umebaini kuwa mmoja kati ya makachero wa Saudi alitoka nje ya ofisi za ubalozi huo akiwa amevalia nguo alizoingia nazo marehemu pamoja na kuvaa ndevu za bandia na nywele za bandia ili afanane naye.

Picha hizo zinamuonesha mtu huyo aliyefanania na Khashoggi akiwa ndani ya mavazi aliyoingia nayo mwandishi huyo, akitoka kwa kutumia mlango wa nyuma ili ionekane kama mwandishi huyo alitoka ndani ya ofisi hizo.

Mtu huyo alionekana kwenye picha za video za CCTV kamera ametajwa kwa jina la Mustafa al-Madani, aliyekuwa sehemu ya kundi la watu waliodaiwa kutekeleza mauaji ya mwandishi huyo ndani ya ofisi hizo.

Mwandishi huyo alifika katika ofisi hizo za ubalozi kuitikia wito wa mwaliko, lakini alikuja na mchumba wake aliyekuwa anamsubiri nje ya ofisi hizo. Hata hivyo, imeripotiwa kuwa mchumba wake huyo ambaye alikuwa mtu wa kwanza kuripoti kupotea kwa mwandishi huyo ndani ya ofisi hizo, alidai kuwa alielekezwa na walinzi kuwa mpenzi wake alitoka kwa kupitia mlango wa nyuma.

Uchunguzi unaonsha kuwa Mustafa al-Madani ambaye alivalia nguo za marehemu ili kuonekana kwenye picha kama ni yeye [Kashoggi] akitoka, alionekana wakati wa kuingia akiwa ndani ya mavazi tofauti na akiwa hana ndevu.

Kutokana na hali hiyo, ametuhumiwa kuwa alikuwa mmoja wa kundi la watu waliotumwa kumuua mwandishi huyo.

Saudi Arabia imekuwa ikitoa matamko tofauti-tofauti ya kukanusha na baadaye kukubali kuhusu mauaji hayo, wiki hii imekiri kuwa Khashoggi aliuawa ndani ya ofisi za ubalozi huo uliopo Istanbul lakini walidai kuwa kifo chake kilitokana na kupigana na mmoja wa makachero.

Jana, waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir aliiambia Fox News kuwa wamebaini Kashoggi aliuawa kimakosa na kwamba hawafahamu mwili wake ulipo.

“Tumejipanga kutafuta ukweli kwa kufukua kila jiwe. Tunalenga kutafuta ukweli mtupu na tunalenga kuwaadhibu wale wote waliohusika na mauaji,” al-Jubeir alisema kwenye mahojiano.

Marekani ambao ni washirika wa Saudi Arabia, umeweka msukumo mkubwa wa kutaka kufahamu ukweli wa mwandishi huyo wa habari. Rais Donald Trump aliahidi kusimamia kidete zoezi hilo hadi Saudi waeleze ukweli, hatua ambayo iliungwa mkono na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 23, 2018
Pacquiao kuzichapa na swahiba wa Mayweather

Comments

comments