Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans linaamini kikosi chao kitatinga Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu, licha ya kupewa nafasi finyu dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Young Africans itaanzia nyumbani Dar es salaam, Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi (Oktoba 08), kisha watakwenda Sudan kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili kati ya Oktoba 14-16.

Kocha Msaidizi wa Young Africans, Cedric Kaze amewatuliza Mashabiki na Wamachama wa klabu hiyo kwa kusema kinaweza kupata ushindi popote, hivyo ana uhakika timu yao itashinda mchezo wa Mkondo wa Kwanza na Pili utakaopigwa ugenini.

“Hatuwezi kusema mchezo wetu uliopita dhidi ya Zalan ulikuwa kipimo sahihi katika mashindano haya, ni kweli tunawaheshimu lakini nadhani kwetu Al Hilal watatupa changamoto nzuri.”

“Tumezungumza na wachezaji wetu kuwakumbusha juu ya hilo, kuhakikisha wanasahau matokeo ya michezo iliyopita na kuanza upya, tutaanzia nyumbani katika mchezo huu, lakini kwa ubora wa kikosi tulichonacho tunaamini tunaweza kupata matokeo mazuri popote na kufuzu hatua inayofuata.” amesema Kaze

Young Africans ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, wamefuzu hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwaondosha Zalan FC ya Sudan Kusini kwa matokeo ya jumla ya mabao 9-0.

Kocha Mgunda: Sijapata mtu maalum safu ya ulinzi
Jupiter kukatiza jirani na uso wa Dunia baada ya miongo sita