Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Simu ya Safaricom, Bob Collymore amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 61, leo asubuhi, Julai 1, 2019 akiwa nyumbani kwake jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Safaricom, Collymore alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ambao amekuwa nao kwa kipindi kirefu na kwamba alikuwa akitibiwa kwenye hospitali mbalimbali ikiwa ni pamoja na Aga Khan jijini humo.

“Kwa huzuni kubwa, tunatangaza kifo cha Afisa Mtendaji Mkuu, William Collymore kilichotokea nyumbani kwake, leo asubuhi, Julai 1, 2019,” imeeleza taarifa ya Safaricom.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, marafiki na wafanyakazi wenzake Collymore.

“Kwa huzuni kubwa, nimepokea taarifa ya kifo cha Afisa Mtendaji Mkuu wa Safaricom, Bob Collymore baada ya kupambana kwa miaka mingi na saratani. Kama nchi, tumempoteza mtendaji muhimu wa kampuni mwenye mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa letu, tutamkumbuka sana,” ujumbe wa Rais Uhuru umesomeka.

Kwa mujibu wa Citizen TV, Clymore alikuwa anafahamu maisha yake yalikuwa yamefikia ukingoni na alikuwa tayari kuifikia siku ya leo ingawa hakuifahamu.

Zitto: Tunafahamu Raphael alipo, Utekaji ni ushamba
‘Wabakaji, wanaowapa mimba wanafunzi wahasiwe’