Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza mkakati mpya wa kuhakiki wanachama wake na kutumia kadi za kieletroniki ili kusimamia vyema mapato na utambuzi wa wanachama wake.

Mkakati huo umetangazwa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe katika kikao cha ndani mkoani Morogoro, kilichowahusisha wananchi wa vijiji na vitongoji pamoja na viongozi mbalimbali wa mkoa huo.

Mbowe alisema kuwa uhakiki na uanzishwaji wa kadi hizo za kieleketroniki utasaidia kuwadhibiti baadhi ya viongozi wasio waaminifu pamoja na kujihakikishia mapato ya takribani shilingi bilioni 13.9 kila mwaka, hali itakayopunguza utegemezi wa ruzuku ya Serikali.

Alisema kuwa kadi hizo zitakuwa zikilipiwa ada ya shilingi 1,000 kwa mwaka na mwanachama na kwamba anaamini mpango huo utafanikiwa kwani kuna baadhi ya sehemu kadi za chama hicho ni lulu na huuzwa hadi shilingi 5,000 badala ya shilingi 500.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kati ya mwaka wa fedha 2009/2010 na 2012/2013, Chadema ilipokea ruzuku ya shilingi bilioni 9.2 huku CCM ikipokea shilingi bilioni 50.97.

CUF ilipokea shilingi bilioni 6.29, NCCR-Mageuzi shilingi milioni 677, UDP shilingi milioni 33, TLP shilingi milioni 217, APPT shilingi milioni 11, DP shilingi milioni 3.3 na Chausta shilingi milioni 2.4.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Susan Kiwanga alisema kuwa wamekuwa wakikumbana na changamoto ya mapato kwakuwa ada za uanachama zimekuwa hazilipwi ipasavyo.

Katika hatua nyingine, Mbowe aliweka wazi mkakati wa chama hicho wa kusimika mizizi katika maeneo ya vijijini, mitaa na vitongoji na balozi za nyumba kumi.

“Kufikia mwaka 2017 kupitia program ya ‘Chadema Msingi’, tumekusudia kujikita zaidi kusaka wanachama kutoka ngazi ya mitaa, vitongoji na balozi na tutaanza uchaguzi ndani ya chama,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa wameamua kufanya hivyo kwakuwa wamebaini hushindwa kufanya vizuri katika chaguzi za wenyeviti wa mitaa na madiwani katika maeneo mengi kwakuwa hukosa misingi imara ya wawakilishi katika ngazi za chini.

Lema agonga mwamba tena mahakamani
Mzunguuko Wa Tano Waunguruma Ulaya